1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Ukraine zatia saini mkataba wa kihistoria

22 Julai 2022

Urusi na Ukraine zimetia saini mkataba wa kihistoria na Umoja wa Mataifa na Uturuki wa kuanzisha tena usafirishaji wa nafaka ambao huenda ukapunguza mzozo wa chakula duniani ambapo mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa.

https://p.dw.com/p/4EWqE
Ukraine-Krieg | Abkommen über Export von ukrainischem Getreide
Picha: Umit Bektas/REUTERS

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu na waziri wa miundombinu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov kila mmoja alitia saini makubaliano tofauti lakini yanayofanana na maafisa wa Umoja wa Mataifa na Uturuki kuhusu kufungua tena njia za usafirishaji katika bahari nyeusi. Haya yameripotiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Maafisa wa Ukraine wamesema hawakutaka kuandika majina yao katika stakabadhi sawa na Urusi kwasababu ya vita kati ya mataifa hayo mawili ambavyo vimedumu kwa miezi mitano sasa.

Guteress ataja makubaliano kuwa ishara ya matumaini

Wakati wa hafla hiyo ya kutia saini makubaliano hayo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa leo kuna ishara ya matumaini katika bahari nyeusi. Ameongeza kuwa ni matumaini, uwezekano na afueni katika dunia vinavyohitajika zaidi kwasasa. Guterres ametoa wito kwa Urusi na Ukraine kutekeleza vilivyo makubaliano hayo. Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuzuia baa la njaa na kupunguza mfumuko wa bei duniani.

Ukraine Interview Mykhailo Podolyak Berater von Präsident Selenskyj
Mykhaylo Podolyak - Msaidizi wa rais wa Ukraine Picha: Anna Fil/DW

Hata hivyo katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, msaidizi wa rais wa Ukraine Mykhaylo Podolyak ameonya kuwa ukiukaji wa Urusi wa makubaliano hayo na uvamizi unaozunguka bandari za Ukraine utakabiliwa na majibu ya haraka ya kijeshi. Makubaliano hayo ya kwanza makubwa kati ya pande hizo mbili zinazohasimiana yametiwa saini wakati vikosi vya Urusi vikishambulia Kusini mwa pwani ya Ukraine na kusababisha vifo vya watu kadhaa katika eneo la viwanda la Donbas. Makataba huo wa usafirishaji nafaka ni maelewano makubwa zaidi kati ya Urusi na Ukraine tangu uvamizi wa Urusi katika taifa jirani la Ukraine mwishoni mwa mwezi Februari. Kulingana na duru za Ukraine, bandari tatu karibu na mji wa Odessa zinahusika.

Urusi yapeleka mashine za uvunaji katika maeneo inayoyathibiti Ukraine

Wakati huo huo, Urusi imepeleka mashine za uvunaji kutoka eneo la Crimea lililoiteka kutoka Ukraine kuelekea maeneo mengine mawili yanayodhibitiwa na Urusi ya  Zaporizhzhia na Kherson nchini Ukraine kuziba nakisi ya vifaa vinavyohitajika kuvuna . Haya ni kwa mujibu wa mamlaka iliyoidhinishwa na Urusi katika maeneo hayo. Ukraine ilikuwa imeituhumu Urusi, muuzaji wa ngano mkubwa zaidi duniani kwa kuiba nafaka kutoka maeneo ambayo jeshi la Urusi limeyateka tangu taifa hilo lilipoivamia Ukraine mnamo Februari 24. Hata hivyo Urusi imekanusha madai hayo.