Upinzani Afrika waipongeza Mahakama ya Juu ya Kenya | Matukio ya Afrika | DW | 04.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Upinzani Afrika waipongeza Mahakama ya Juu ya Kenya

Viongozi wa upinzani barani Afrika wamesifia hatua ya mahakama ya juu nchini Kenya kutengua matokeo ya urais ya uchaguzi uliofanyika August 8, mwaka huu yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta.

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai aliwaeleza maelfu ya wafuasi wake katika mkutano wa hadhara mwishoni mwa wiki kuwa   iwapo hilo limefanyika Kenya  basi linaweza kufanyika Zimbabwe pia.

 Tsvangirai ambaye ni kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) amejaribu mara tatu kuwania nafasi ya urais kupitia chaguzi zilizofanyika nchini Zimbabwe lakini amekuwa akishindwa katika chaguzi hizo na Rais Robert Mugabe ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1980.

Chaguzi nchini Zimbabwe mara nyingi zimekuwa zikigubikwa na vurugu, vitisho na mashitaka ya ukiukwaji wa tararibu za uchaguzi. Tshangirai amesema  huu ni mfano wa kuigwa barani Afrika  na kuwa ni hatua moja nzuri katika kufikia demokrasia ya kweli barani Afrika.

Simbabwe (DW/C. Mavhunga )

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai

Ijumaa iliyopita mahakama ya juu ya Kenya ilifuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Novemba 8 yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta  kufuatia mahakama hiyo kuthibitisha kasoro nyingi katika zoezi la uchaguzi huo na kuagiza uchaguzi  ufanyike baada ya siku 60 ambapo sasa uchaguzi huo unatararajiwa kufanyika  Oktoba 31 mwaka huu.

" Majaji wa Kenya wametoa fundisho barani Afrika na duniani kwa ujumla" alisema kiongozi wa upinzani nchini Burundi Charles Nditije.

Burundi inakabiliwa na  mgogoro wa kisiasa tangu April 2015 wakati Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kuwania muhula wa tatu wa uongozi ambapo alishinda uchaguzi uliofanyika mwezi Julai uliosusiwa na upinzani  wakidai kuwa ni ukiukaji wa katiba.

 Nditije  anayeoongoza muungano wa vyama vya upinzani - CNARED alisema kilichofanyika Kenya ni tofauti na yaliyotokea nchini Burundi na kusisitiza kuwa uamuzi wa mahakama ya juu ya Kenya ni mfano mzuri wa uhuru wa mahakama unaotakiwa kuigwa.

Upinzani Uganda nao wasifia mahakama ya juu ya Kenya

 Uganda ambayo iko chini ya utawala wa Rais Yoweri Kaguta Museveni  tangu mwaka 1986 kiongozi wa chama cha upinzani nchini humo Kizza Besigye  alipongeza uamuzi wa mahakama ya juu ya Kenya akisema ni mfano wa kuigwa barani Afrika .  Besigye alitiwa mabaroni, wakati na baada ya uchaguzi wa Februari mwaka 2016 ambapo alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliogubikwa na utata.

Ugandas Oppositionsführer Kizza Besigye (DW/E. Lubega)

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye

Museveni anayeliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 31 alishinda duru ya kwanza  ya uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa lakini hata hivyo waangalizi wa uchaguzi kutoka nje  walisema uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya vitisho na kuongeza kuwa ushindi wa Museven ulitokana na udanganyifu na vitisho.

Nchini Tanzania mbunge wa upinzani nchini humo Zito Kabwe alitoa mwito wa kufanyika kwa marekebisho ya katiba nchini humo akisema Kenya imepiga hatua kubwa  na kuwa Tanzania inahitaji katiba mpya ili kuwepo na uwezekano wa kupinga matokeo ya uchaguzi kupitia mahakama.

Nchini  Rwanda  ambako Rais Paul Kagame alichaguliwa  tena kushika muhula wa tatu  kwa asilimia 99 ya kura mwezi uliopita,Kiongozi wa upinzani Frank Habineza alisema uamuzi wa mahakama ya juu ya Kenya unatia moyo kwa upinzani barani Afrika. Alisema uhuru wa mfumo wa mahakama ni munhimu barani Afrika  na unasaidia kuzuia hatua nyingine mbadala za kupinga matokeo hayo kama vile kuanzisha makundi ya upinzani yenye silaha  ili kudai haki.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com