1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Vita vya Ukraine kusababisha mgogoro wa chakula duniani

Bruce Amani
19 Mei 2022

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unawez kusababisha uhaba wa chakula duniani katika miezi ijayo. Mkuu wa umoja huo amesema vita hivyo vimezidisha uhaba wa chakula katika mataifa maskini zaidi

https://p.dw.com/p/4BUrp
Ukraine Ernte in der Donetsk Region
Picha: Nikolai Trishin/TASS/picture alliance/dpa

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine huenda ukasababisha uhaba wa chakula duniani katika miezi ijayo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema vita hivyo vimezidisha uhaba wa chakula katika mataifa maskini zaidi kutokana na kupanda kwa bei. 

Soma pia: Urusi yaushambulia mji wa Odesa

Guterres amesema anafanya kile alichokiita kuwa ni mawasiliano ya mfululizo na Urusi, Ukraine, Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya katika jaribio la kurejesha uuzaji wa nafaka ya Ukraine wakati mgogoro wa chakula duniani ukizidi kuwa mbaya zaidi.

Antonio Guterres | UN Generalsekretär
Guterres amesema kuna mengi ya kufanywa kupata jibuPicha: Eskinder Debebe/UN Photo/Xinhua/imago images

Akiuhutubia mkutano wa ngazi ya mawaziri kuhusu chakula mjini New York, Guterres ameiomba Urusi kuruhusu usafirishaji salama wa nafaka iliyohifadhiwa katika bandari za Ukraine na chakula cha Urusi na mbolea kufikishwa kikamilifu na bila vizuizi kwa masoko ya ulimwengu.

Vita vya Urusi nchini Ukraine vimesababisha bei za kimataifa za nafaka, mafuta ya kupika, nishati na mbolea kupanda, na Guterres ameonya kuwa hiyo itafanya mizozo ya chakula, nishati na kiuchumi katika nchi maskini kuwa mbaya zaidi. "Mgogoro wa chakula hauheshimu mipaka, na hakuna nchi inayoweza kuutatua peke yake. Fursa yetu pekee ya kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka kwenye njaa ni kuchukua hatua pamoja, haraka na kwa mshikamano." Amesema.

Soma pia: Zelensky ataka bandari za Ukraine zifunguliwe

Guterres ambaye alizuru Moscow na Kyiv mwezi uliopita, amesema ana matumaini ya kupatikana suluhu lakini safari bado ni ndefu.

Urusi na Ukraine kwa pamoja zinachangia karibu theluthi moja ya bidhaa za ngano duniani. Ukraine pia ni muuzaji mkubwa wa mahindi na mafuta ya alizeti, wakati Urusi na Belarus zikichangia zaidi ya asilimia 40 ya mbolea duniani.

Odesa Hafen
Bandari ya Odesa imefungwa kutokana na vita UkrainePicha: imago images/unkas_photo

David Beasley, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani – WFP, ameonya kuwa kushindwa kuzifungua bandari za Ukraine itakuwa ni kutangaza vita kwa upatikanaji wa chakula duniani, na hivyo kusababisha njaa na kuyumbishwa kwa mataifa pamoja na mmiminiko wa wahamiaji.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken ambaye aliuongoza mkutano huo, ameziomba nchi kutoa michango mipya muhimu kwa mashirika ya kiutu yanayopambana na uhaba wa chakula, na kuzitaka nchi zenye hifadhi kubwa ya nafaka na mbolea pia kujitokeza mara moja.

Marekani ilitangaza dola bilioni 2.3 kwa ajili ya msaada wa dharura wa chakula tangu Urusi ilipoivamia Ukraine na kuongeza dola milioni 215 zaidi Jumatano, na hivi karibuni Bunge la Marekani linatarajiwa kuidhinisha karibu dola bilioni 5.5 za ufadhili wa ziada kwa ajili ya msaada wa kiutu na chakula.

Soma pia: WFP yaonya mzozo wa Ukraine na Urusi huenda ukaathiri bei za bidhaa nchini Yemen

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Urusi sio tu inafanya vita vyake vya kikatili kwa kutumia vifaru, makombora na mabomu. Urusi inatumia silaha nyingine hatari zaidi na ya kimya: njaa na kuwanyima watu mahitaji ya msingi.

AFP, Reuters