1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky atoa wito bandari za Ukraine zifunguliwe

Josephat Charo
10 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito hatua zichukuliwe kuzifungua bandari nchini mwake kuepusha mzozo wa chakula duniani. Zelensky amesema biashara katika bandari hizo imesimama

https://p.dw.com/p/4B3zc
Ukraine | Präsident Selenskyj
Picha: John Moore/Getty Images

Zelensky amesema biashara katika bandari zilizozingirwa na Urusi imesimama na kuitaka jumuiya ya kimataifa ichukue hatua za haraka kufikisha mwisho hatua ya Urusi kuzizingira ili kuruhusu usafirishaji wa ngano. Rais huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuzungumza na rais wa baraza la Ulaya Charles Michel ambaye alikuwa akzuru mji wa Odesa, bandari muhimu katika bahari Nyeusi kwa usafirishaji wa mazao ya kilimo

Makombora yamepiga maeneo ambayo ni vivutio vya utalii katika mji wa bandari wa Odesa na kuharibu majengo matano na kuwajeruhi watu wawili. Maafisa wa serikali ya manuspaa wamesema milipuko iliyotokea imesababisha moto katika eneo la maduka. Hakuna taarifa za vifo zilizotolewa.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa watu wanne wameuwawa na nyumba kadhaa kuharibiwa katika mashambulizi ya Urusi katika mji wa Bogodukhov, kaskazini magharibi mwa mji wa Kharkhiv, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine.

Wizara ya ulinzi wa Ukraine imesema vikosi vya Urusi vikisaidiwa na vifaru na silaha nzito vilikuwa vikifanya operesheni ya uvamizi katika kiwanda cha Azovstal mjini Mariupol, ambako mamia ya wapiganaji wa Ukraine wamenasa kwa miezi kadhaa ya kuzingirwa eneo hilo. Raia waliokuwa wakijihifadhi mahala hapo waliondolea siku chache zilizopita.

Petro Andryuschenko, mpambe na mshauri wa meya wa mji wa Mariupol, amesema wanajeshi wa Urusi walikuwa wakijaribu kulipua daraja moja linalotumiwa kuwahamisha watu, kwa lengo la kuwanasa wapiganaji wa mwisho waliosalia ndani ya kiwanda hicho.

Wakati hayo yakiarifiwa rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaahidi raia wa Ukraine watashinda vita dhidi ya Urusi. Katika hotuba yake aliyoitoa jana siku ya ushindi dhidi ya manazi, Zelensky alisema wanapigania ushindi mpya na licha ya kwamba njia ni ngumu, hapana shaka watashinda.

Ukraine, Odesa | Zerstörtes Grande Pettine Hotel
Picha: Max Pshybyshevsky/AP/dpa/picture alliance

Waziri wa ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amesema hakuwezi kuwa na siku ya ushindi kwa Warusi bali ni aibu tu na bila shaka watashindwa nchini Ukraine.

Marekani kuisaidia Ukraine na dola bilioni 40

Huko nchini Marekani rais wa Marekani Joe Biden jana Jumatatu alifufua hatua ya enzi ya vita vya pili vya dunia iliyotumiwa kuimarisha washirka wa Marekani waliokuwa wakipigana na Ujerumani ya manazi, kuiruhusu serikali kuharakisha usafirishaji wa silaha kwa Ukraine katika vita vyake dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Biden amesaini muswada wa sheria akisema Marekani inawaunga mkono raia wa Ukraine wanaopigana kuilinda nchi yao na demokrasia yake dhidi ya vita vya kinyama vya rais wa Urusi Vladimir Putin. Biden pia ameashiria yuko tayari kufanya makubaliano ya kisiasa katika bunge la Marekani Congress ili aungwe mkono apate ridhaa ya haraka ya fedha nyingine kiasi cha dola bilioni 33 kwa kuisaidia Ukraine.

Awali Biden alikuwa ametaka kuidhinishwa kwa fedha hizo kuambatane na msaada wa fedha kwa serikali katika mpango wa kupambana an ugonjwa wa Covid-19, lakini kwa sababu wanasiasa wa chama cha Republican wanajivuta na kuuchelewa mchakato huo kuidhinisha fedha za kupambana na Covid, Biden amesema yuko tayari kuachana na madai ya kutaka fedha za Covid kwa sasa na anataka apate tu fedha kwa ajili ya Ukraine.

Mjini Washington wanasiasa wa chama cha Democatic bungeni wanaandaa mpango utakaoimarisha kiwango cha dola bilioni 33 za Kimarekani kwa ajili ya vita vya Ukraine hadi kufikia dola bilioni 40 kama msaada wa kijeshi na kibinadamu na kura inatarajiwa kupigwa bungeni hivi leo Jumanne.

afpe,reuters, ap