1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yatikiswa na Brexit

Yusra Buwayhid27 Juni 2016

Uingereza imetumbukia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Jumapili iliyopita kuamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya kupitia kura ya maoni huku viongozi wa mataifa ya bara hilo wakiwa katika hali ya kuchanganyikiwa.

https://p.dw.com/p/1JEI9
Britische europäische und Deutsche Flagge Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/A. Arnold

Viongozi wa nchi zilizo na nguvu katika Umoja wa Ulaya za Ujerumani, Ufaransa na Italia wanakutana leo hii na rais wa umoja huo Donald Tusk mjini Paris na baadae mjini Berlin Ujerumani kujadili hatua ya Uingereza kujitoa katika umoja huo, ikiwa ni siku mbili kabla ya kufanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa umoja huo mjini Brussels, Ubelgiji.

Tusk anategemewa kukutana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande mjini Paris na wote wawili baadae wanategemewa kukutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi kwa majadiliano zaidi juu ya suala hilo mjini Berlin.

Mchakato wa miaka miwili wa kujiondoa Umoja wa Ulaya utaanza pale waziri mkuu wa Uingereza atakapoitekeleza ibara ya 50 ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya wa Lisbon. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ataweza kufanya hivyo atakapokutana na viongozi wengine 27 wa nchi wanachama wa umoja huo mjini Brussels hapo kesho. Hata hivyo Cameron ameashiria kuwa angependa kungoja kwa miezi kadhaa kabla ya kuanzisha mchakato rasmi wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Armenien Papst Franziskus
Picha: picture alliance/dpa/T. Fabi

Papa Francis asema upepo wa mgawanyiko wavuma

Halikadhalika kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis siku ya Jumapili ameeleza wasiwasi wake juu ya mustakbali wa Umoja wa Ulaya na kusema upepo wa mgawanyiko unavuma barani humo.

"Yote haya lazima yatufanye tutafakari zaidi, ni kweli nchi yangu imo ndani ya Umoja wa Ulaya, lakini nataka kuwa na baadhi ya mambo ambayo ni yangu, yanayoendana na utamaduni wangu, na Umoja wa Ulaya unatakiwa kutoa uhuru zaidi kwa nchi wanachama, lazima uanze kufikiria mfumo mpya wa kuunganisha nchi za Ulaya, na pia wajaribu kuwa wabunifu zaidi katika kutengeneza ajira," amesema Papa Francis.

Kamishna wa Ujerumani kwa Umoja wa Ulaya Guenther Oettinger ameiambia redio ya Ujerumani Deutschlandfunk kwamba chama cha Uingereza kinachoongoza serikali cha Conservative kinatakiwa kufanya maamuzi ya haraka kutokana na kwamba kila siku zikisonga mbele wasiwasi nao unazidi kusambaa, huku kukiwa na hatari ya wawekezaji duniani kote kuanza kukata tamaa ya kuwekeza Uingereza pamoja na kupoteza imani na Umoja wa Ulaya.

Kwa upande wa mahusiano kati ya Ufaransa na Uingereza, mameya wa miji ya London na Paris wameahidi kuendelea kufanya kazi pamoja kuijenga karne iyayo licha ya uamuzi wa Uingereza wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/dpa/eafpe

Mhariri:Yusuf Saumu