1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUjerumani

Ujerumani yakabiliwa na mdororo wa kiuchumi

Saleh Mwanamilongo
25 Mei 2023

Uchumi wa Ujerumani umeporomoka kwa asilimia 0.3 katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2023, kulingana na takwimu zilizotolewa Alhamisi.

https://p.dw.com/p/4Rp7O
Uchumi wa Ujerumani umeporomoka kwa asilimia 0.3 katika robo ya kwanza ya mwaka huu
Uchumi wa Ujerumani umeporomoka kwa asilimia 0.3 katika robo ya kwanza ya mwaka huu Picha: Daniel Roland/AFP

Mdororo huo ulikuja wakati Ujerumani ikipambana na kupanda kwa bei ya nishati kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambao umeathiri kaya na biashara. Kuongezeka kwa gharama ya nishati kumesababisha mfumuko wa bei, ambao ulifikia hadi asilimia 7.2 nchini Ujerumani mnamo Aprili, chini kidogo kutoka kilele chake mwishoni wa 2022.

Idara ya taifa ya Takwimu, Destatis,imesema leo kwamba kupanda kwa bei kuliendelea kuwa mzigo kwa uchumi wa Ujerumani mwanzoni mwa mwaka. Athari hiyo ilihisiwa haswa na watumiaji ambao walidhibiti matumizi yao kwenye vitu kama vile chakula na mavazi.

Jens-Oliver Niksasch, mchambuzi wa benki ya LBBW amesema marekebisho hasi ya takwimu ya ukuaji hayakuwa ya kushangaza kufuatia msururu wa viashirio dhaifu vya kiuchumi hapa nchini Ujerumani. Niklasch amesema viashiria vya mapema vinapendekeza kwamba mambo yataendelea kuwa dhaifu vile vile katika robo ya pili ya 2023.

''Ujerumani imefanya vya kutosha''

Kansela wa Scholz amesema mtazamo wa kiuchumi wa Ujerumani ulikuwa "mzuri sana"
Kansela wa Scholz amesema mtazamo wa kiuchumi wa Ujerumani ulikuwa "mzuri sana"Picha: Christopher Furlong/Getty Images

Maagizo ya viwanda, ambayo yanatoa ladha ya mazao ya kiwanda, yalipungua Machi ikilinganishwa na mwezi huo huo mwaka jana. Ujerumani, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea sana uagizaji wa nishati ya Urusi, ilijikuta katika hali ngumu kufuatia uvamizi wa Urusi mnamo Februari mwaka jana.

Takwimu hizo za kuporomoka kwa uchumi wa Ujerumani zitawapa changamoto watunga sera mjini Berlin ambao mwezi Aprili waliinua utabiri wao wa ukuaji wa uchumi mwaka 2023 hadi asilimia 0.4, huku kukiwa na matumaini ya mwaka wa mapema.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz hapo awali aliashiria kwamba Ujerumani ilikuwa imefanya vya kutosha kukabiliana na mdororo wa kiuchumi. Mara ya mwisho Ujerumani kushuhudia mdodoro wa kiuchumi ilikuwa mwaka 2020 wakati wa janga la Corona.

Hisa za dunia ziliporomoka Alhamisi huku wawekezaji wakitazama dalili za maendeleo katika mpango wa kuzuia kutolipa deni la serikali ya Marekani. Bei ya mafuta ilishuka, pipa hii leo liliuzwa thamani ya dola 77.5 , wakati bei ya gesi ya Ulaya pia ilishuhudiwa kuporomoka hadi karibu kiwango cha chini mnamo kipindi cha takriban miaka miwili.