1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Von der Leyen mit EU-Kommission zu Gesprächen in Kiew
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakiwa na wenzao wa Ukraine mjini Kyiv.Picha: Ukraine Presidency/dpa/picture alliance

Ujerumani yaidhinisha kutumwa vifaru chapa Leopard 1 Ukraine

Mohammed Khelef
3 Februari 2023

Ujerumani imeidhinisha rasmi kutumwa vifaru chapa Leopard 1 nchini Ukraine kuisaidia kwenye vita vyake na Urusi, huku viongozi wa Umoja wa Ulaya wakikutana na wenzao wa Kyiv kujadiliana msaada na vikwazo zaidi kwa Urusi.

https://p.dw.com/p/4N4b0

Taarifa kutoka makao makuu ya nchi mjini Berlin ilisema tayari serikali imeidhinisha vifaru hivyo kupelekwa Ukraine, ikiwa ni jibu la wito wa Kyiv inayosaka silaha za kiwango cha juu kukabiliana na vikosi vya Urusi. 

Bila ya kueleza undani zaidi, msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Hebestreit, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa (Februari 3) kwamba angeliweza kuthibitisha kwa uhakika kabisa kwamba kibali cha kutumwa vifaru hivyo kimeshatolewa. 

Soma zaidi: Putin aonya nchi za magharibi dhidi ya kuipa Ukraine silaha

Idhini hii ya Ujerumani kutuma vifaru hivyo ambavyo vinachukuliwa kuwa mojawapo ya zana za kisasa na za hali ya juu kijeshi ulimwenguni, ilitolewa siku moja tu baada ya mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, kusema kuwa asingelishangazwa endapo Ujerumani na Marekani zingebadilisha misimamo yao ya kutotuma silaha kali za kivita nchini Ukraine.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waonesha mshikamano

Von der Leyen mit EU-Kommission zu Gesprächen in Kiew
Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen (kushoto), akizungumza na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine mjini Kyiv.Picha: Uncredited/Ukrainian Presidential Press Office/AP/dpa/picture alliance

Kwenyewe mjini Kyiv, viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya, akiwemo mkuu wa kamisheni na mwenyekiti wake, walikutana na wenzao wa Ukraine katika mkutano ulioangaliwa kama ishara ya mshikamano na uungaji mkono wao kwa Ukraine, wakati huu ukikaribia mwaka mmoja tangu uvamizi wa Urusi uanze mnamo tarehe 24 Februari 2022.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alisema mkutano huu unamaanisha mengi kwa nchi yake na unaashiria jinsi Ulaya ilivyojitolea kushirikiana nao kwa hali na mali.

Soma zaidi: Viongozi wa EU wakutana na rais Volodymyr Zelenskiy

"Kwa mara ya kwanza, serikali ya Ukraine na Kamisheni ya Ulaya wanakaa kitako kupitia kwa kina kila nyanja ya ushirikiano wetu. Hiyo inamaanisha mafungamano zaidi na Umoja wa Ulaya katika viwango vya kitaasisi na binafsi. Inamaanisha kukaribia zaidi Ukraine ndani ya Umoja wa Ulaya. Inamaanisha vikwazo zaidi kwa Urusi kama mchokozi." Alisema.

Kwa upande wake, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, alisema mkutano huu wa kilele unahusu sio tu msaada na mshikamano na Ukraine wakati huu wa vita, bali hata hali ya Ukraine baada ya vita kumalizika: 

"Ni mjadala kamili kwa kila jambo linalohusu mahusiano baina ya Umoja wa Ulaya na Ukraine, sio tu kuhusu kuisaidia kupambana na uvamizi wa Urusi, sio tu kuhusu vita hivi, bali pia juu ya hali itakavyokuwa baada ya vita."

Soma zaidi: Kamisheni ya EU yaahidi msaada mpya kwa Ukraine

Rais Volodymyr Zelensky alitazamiwa kuutumia mkutano huu kusisitiza kuharakishwa kwa mchakato wa kuiingiza nchi yake kwenye Umoja wa Ulaya.

Umoja huo ulishapokea maombi ya Ukraine kitambo lakini umekuwa ukisita kuchukuwa hatua za kuharakisha kutokana na tafauti iliyopo miongoni mwa mataifa wanachama.