1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Kenya zasimama kidete kuulinda Umoja wa Mataifa

21 Januari 2026

Kenya na Ujerumani zimeungana kutoa msimamo thabiti kuhusu umuhimu wa kuimarisha Umoja wa Mataifa kama taasisi kuu ya kimataifa inayosimamia amani, usalama na utatuzi wa migogoro duniani.

https://p.dw.com/p/57CS8
Kenya | Nairobi 2026 | Johann Wadephul | Musalia Mudavadi |
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul kwenye mkutano na Waziri Kiongozi wa Kenya Musalia Mudavadi mjini NairobiPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Ujerumani na Kenya zimeweka wazi msimamo wao kuhusu umuhimu wa kuimarisha Umoja wa Mataifa kama nguzo kuu ya usimamizi wa amani na utatuzi wa migogoro duniani, wakati kukiwa na wasiwasi unaotokana na taarifa kwamba Rais wa Marekani Donald Trump anapanga kuanzisha chombo kipya cha kimataifa kitakachoshughulikia masuala ya amani.

Kauli hizo zimetolewa leo jijini Nairobi baada ya mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul na Waziri Kiongozi wa Kenya ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi. 

Wadephul amesisitiza kuwa licha ya changamoto zinazoikabili Umoja wa Mataifa, bado taasisi hiyo ndio yenye uhalali wa kimataifa na inayotambulika kisheria katika kusimamia juhudi za kudumisha amani duniani.

Akizungumza baada ya mkutano na Waziri Kiongozi wa Kenya ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi, Wadephul amesema kuwa pande hizo mbili zimekubaliana kuongeza kasi ya majadiliano ya kisiasa, hususan katika masuala yanayohusu usalama wa kikanda, diplomasia ya kimataifa na uthabiti wa kisiasa.

Wadephul: Dunia inahitaji taasisi imara na zinazotambulika kimataifa

Amesisitiza kuwa mazungumzo ya wazi na ya mara kwa mara kati ya Kenya na Ujerumani ni muhimu katika kujenga misingi imara ya ushirikiano wa muda mrefu.

"Tumekubaliana kuimarisha mazungumzo yetu ya kisiasa, pamoja na kujadili masuala muhimu yanayohusu uthabiti wa kikanda na kimataifa. Kenya ina jukumu muhimu kama mpatanishi katika eneo hili na inabeba wajibu mkubwa katika masuala ya amani na usalama nchini Somalia na Haiti."

Mudavadi, kwa upande wake, amesema badala ya kuanzisha mifumo mipya inayoweza kuleta mgawanyiko au kudhoofisha uratibu wa kimataifa, juhudi zinapaswa kuelekezwa katika kuimarisha taasisi zilizopo kama Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa Kenya haijapokea mwaliko wa kujiunga na chombo kipya kinachoitwa Baraza la Amani, ambacho kinatajwa kuanzishwa na Marekani.

Ama kuhusu ziara ya Wadephul nchini Kenya, Mudavadi amesema ziara hiyo ni ishara tosha ya ushirikiano wa muda mrefu unaozidi kuimarika kati ya mataifa hayo mawili.

"Ziara hii kwa hivyo ni uthibitisho wazi wa uhusiano mzuri na wenye manufaa kwa pande zote, uhusiano unaojengwa juu ya misingi ya pamoja ya demokrasia, kuheshimu sheria za kimataifa na dhamira ya pamoja ya kuendeleza utaratibu wa dunia ulio wa haki, wa amani na endelevu."

Kenia Nairobi 2026 | Außenminister Johann Wadephul pflanzt Baum im Ausbildungszentrum für Friedensunterstützung
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul akipanda mti alipotembelea Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Misaada ya Kibinadamu (HPSS)Picha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Kauli za Wadephul na Mudavadi kuhusu kuimarisha Umoja wa Mataifa zinatokana na hatua ya Trump kuanzisha baraza hilo jipya ambalo linatarajiwa kusimamia ujenzi upya wa Ukanda wa Gaza baada ya vita.

Hata hivyo, hati ya uanzishwaji wa baraza hilo imeibua hofu kwamba linaweza kupanua majukumu yake hadi kwenye migogoro mingine duniani, hatua ambayo inaweza kuleta changamoto kubwa kwa Umoja wa Mataifa na kuibua maswali kuhusu mustakabali wa mfumo wa kimataifa wa usimamizi wa amani.

Wadephul amekiri kuwa Umoja wa Mataifa inahitaji mageuzi ili kuendana na changamoto za sasa, lakini ameweka wazi kwamba mageuzi hayo yanapaswa kufanyika ndani ya mfumo uliopo. Ameongeza kuwa Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, anatarajiwa kutafuta ufafanuzi zaidi kuhusu Baraza hilo la Amani wakati wa mkutano wa mwaka huu wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaoendelea mjini Davos.

Wadephul kufanya ziara Ethiopia

Ziara ya Wadephul katika ukanda wa Afrika Mashariki ni ya siku mbili, ikijumuisha Kenya na Ethiopia.

Ziara ya Wadephul nchini Kenya ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Akiwa Nairobi, mbali na kukutana na Mudavadi, anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais William Ruto.

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, mazungumzo hayo yataangazia masuala ya uhusiano wa pande mbili, usalama wa kikanda na kimataifa, pamoja na umuhimu wa kulinda utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria.

Kenya Nairobi 2026 | Johann Wadephul
Johann Wadephul akiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini NairobiPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Katika ratiba yake nchini Kenya, Wadephul anatarajiwa pia kutembelea kituo cha mafunzo ya amani pamoja na taasisi ya elimu inayoendeshwa na kampuni ya Kijerumani, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kiusalama kati ya mataifa hayo mawili.

Kesho Alhamisi, Waziri huyo ataelekea Addis Ababa, Ethiopia, kwa mazungumzo ya kisiasa na ziara katika makao makuu ya Umoja wa Afrika AU ambako atajadili masuala ya ushirikiano wa bara la Afrika na Ujerumani pamoja na changamoto za usalama katika eneo la Pembe ya Afrika.