Ujerumani kukwaana na Uswisi, Havertz arudi kikosini
27 Machi 2026
Hii ni baada ya mshambuliaji huyo wa Arsenal kutajwa katika kikosi kitakachoanza mechi ya kirafiki ya Ujerumani dhidi ya Uswisi Ijumaa.
Mabeki wa kati Jonathan Tah na Nico Schlotterbeck pia wataanza mechi hiyo huku Angelo Stiller na Leon Goretzka wakitarajiwa kuanza kama viungo wakabaji.
Kulingana na kocha mku Julian Nagelsmann,mlinda lango wa Bayern Munich Jonas Urbig mwenye umri wa miaka 22, alilazimika kuondoka kwenye kambi ya timu ya taifa baada ya kupata jeraha dogo la goti, hivyo atakosa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza katika timu ya taifa.
Katika mechi hiyo, Ujerumani na Uswisi zimekubaliana kuwa wanaweza kufanya mabadiliko ya hadi wachezaji 11 kwa kila timu.
Wamefikia makubaliano hayo kutokana na uamuzi uliotolewa na Bodi ya Kimataifa ya Kandanda, IFAB, mwishoni mwa mwezi Februari.
Bodi hiyo ambayo inatunga sheria za kandanda ilisema timu zinaweza kubadilisha hadi wachezaji 8 katika mechi za kirafiki za kimataifa ila endapo zitakubaliana idadi ya juu zaidi ya hadi wachezaji 11 ni jambo linalowezekana.
Kocha wa Uswisi Murat Yakin amethibitisha kwamba atafanya mabadiliko 11 ili aweze kuwatumia wachezaji wengi zaidi iwezekanavyo, anaotazamia kuwatumia katika kombe la dunia.