1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiNigeria

Ujerumani kufanya biashara ya nishati na Nigeria

Hawa Bihoga
30 Oktoba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekutana na Rais wa Nigeria Bola Tinubu jana Jumapili kujadili fursa za biahsra na uwekezaji, wakati wa ziara yake ya Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/4YC82
Kansela wa Ujerumani  Olaf Scholz  akiwa na rais wa Nigeria Bola Tinubu
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwa na rais wa Nigeria Bola TinubuPicha: Nosa Asemota/Nigeria State House/AP/picture alliance

Katika ziara yake ya tatu barani Afrika tangu alipoingia madarakani mwaka 2021, na ya pili mwaka huu, Kansela Scholz aliunga mkono kuendeleza zaidi uwezo wa Nigeria kukidhi mahitaji ya ndani hata wakati Ujerumaniinatafuta kuboresha uhusiano wa kibiashara na mshirika wake wa pili kwa ukubwa wa kibiashara katika kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kansela Scholz alimuambia Rais Tinubu wakati wa mkutano wao mjini Abuja kwamba mambo makuu ya ushirikiano wa nchi hizo mbili yanahusisha ushirikiano na Nigeria kusaidia kushughulikia masuala ya kikanda na kimataifa kama vile uhamiaji, usalama na mapinduzi yaliyokithiri katika kanda za Afrika Magharibi na Kati.

Alisema kuna fursa  nyingi sio tu kutokana na gesi na mafuta ambavyo kijadi vinahusishwa na nchi ya Nigeria, lakini palipo na nafasi kubwa ya kuboresha na kutumia vyema uwezo wa Nigeria.

"Lakini pia kuingia katika uwekezaji kwa ajili ya siku zijazo, unaohusu hidrojeni na mambo yote muhimu kwa uchumi."

Soma pia:Scholz asema Ujerumani iko tayari kuekeza Nigeria

Scholz aliongeza kwa kumwambia Tinubu huku akitetea nishati ya haidrojeni inayotazamwa kamarafiki wa mazingirakwamba, Nigeria  inaweza kuzalisha bidhaa zote muhimu kwa watu bila kuharibu mazingira.

Wataalamu wameilezea Afrika kama bara lenye uwezo wa kusafirisha nishati ya hidrojen katikati mwa miito ya kubadili nishati.

Shinikizo kwa Scholz dhidi ya uhamiaji

Kiongozi huyo wa Ujerumani ambaye amekabiliwa na shinikizo kubwa nyumbani kuhushughulikia masuala yanayohusiana na uhamiaji kwenda Ujerumani, amependekeza usimamizi wa pamoja wa suala hilo ambalo linazinufaisha nchi hizo mbili.

Kabla ya kukutana na Tinubu, Scholz aliliambia gazeti la Punch la mjini Lagos kwamba Ujerumani ina mahitaji makubwa ya gesi asilia, na viwango vikubwa vinapaswa kukubaliwa wakati wa majadiliano kati ya wazalishaji wa gesi wa Nigeria na wafanyabiashara wa gesi wa Ujerumani.

Ujerumani: Rasimu ya kuwarudisha watu katika mataifa yao

Mwaka uliyopita, biashara kati ya Ujerumani na Nigeria iliongezeka kwa asilimia 50 hadi kufikia euro bilioni 3, na Scholz amesema bado kuna mengi ya kufanya.

Nigeria ina hifadhi kubwa zaidi ya gesi Afrika, ikikadiriwa kuwa na futi za ujazo trilioni 202, na imeonyesha nia ya kufanya kazi kusaidia kukidhi mahitaji ya Ulaya baada ya Urusi kupunguza pakubwa usambazaji wa gesi asilia kufuatia vita vyake nchini Ukraine.

Soma pia:Scholz: Ujerumani kukuza mahusiano ya kibiashara na Nigeria

Rais wa Nigeria Bola Tinubu kwa upande wake alisema alikuwa na majadiliano mazuri na Kansela Scholz kuhusu uwekezaji wa gesi, na kuomba msaada wa Ujerumani katika kushughulikia changamoto za usalama na uchumi.

Kansela Scholz pia alikutana na Omar Alieu Touray, rais wa Kamisheni ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, nawalijadili mapinduzi ya hivi karibuni katika maeneo ya Afrika.

Hii leo Scholz atafunga mkutano wa biashara kati ya Ujerumani na Nigeria mjini Lagos, kabla ya kuelekea Ghana ambako atakamilisha ziara yake kesho Jumanne.