1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania, Ireland na Norway zaitambua rasmi Palestina

28 Mei 2024

Uhispania, Ireland na Norway zimeitambua rasmi Palestina, katika uamuzi ulioratibiwa ambao Israel imeutaja kuwa 'zawadi kwa Hamas', zaidi ya miezi saba tangu ilipoanzisha vita dhidi ya kundi hilo katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4gODd
Iraland yalitambua rasmi taifa la Palestina.
Ireland pamoja na Norway na Uhispania zimchukuwa hatua ya kihistoria kutambua rasmi taifa la Palestina.Picha: Artur Widak/NurPhoto/picture alliance

Baada ya serikali ya Ireland kuidhinisha rasmi hatua hiyo, Waziri Mkuu Simon Harris alisema lengo ni kuweka hai matumaini ya amani ya Mashariki ya Kati.

Harris alisema walitaka kuitambua Palestina mwishoni mwa mchakato wa amani, lakini wamechukua hatua hiyo pamoja na Uhispania na Norway ili kuweka hai muujiza wa amani, huku akiitolewa wito Israel kukomesha janga la kibinadamu Gaza.

Baada ya utambuzi wa Norway kuanza kutekelezwa, Waziri wa Mambo ya Nje Espen Barth Eide alipongeza hatua hiyo na kuitaja Jumanne hii kuwa siku maalum kwa uhusiano wa Norway na Palestina.

Soma pia: Norway, Ireland, Uhispania kutambua taifa la Palestina

Na baada ya baraza la mawaziri la Uhispania kuunga mkono hatua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje Jose Manuel Albares alisema ni siku ambayo itaangaziwa katika historia ya Uhispania.

Hapo awali, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alisema utambuzi huo ni muhimu kwa amani, akisisitiza kwamba hatua hiyo haijachukuliwa dhidi ya Israel na kwamba ndiyo njia pekee ya kuhakikisha mustakabali wa mataifa mawili yanayoishi bega kwa bega kwa amani na usalama.

Videostill | Ireland, Norway, Uhispania zaitambua rasmi Palestina.
Uhispania, Ireland na Norway zimeanza kulitambua rasmi taifa la Palestina, Jumanne 28, 2024.Picha: Rebecca Ritters/DW

Umuhimu wa kisheria na kisiasa

Profesa Msaidizi wa sheria ya haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya umma katika Chuo Kikuu cha Utrecht, Kushtrim Istrefi, alisema utambuzi huo una "umuhimu wa kisheria na kisiasa na sio ishara tu" na mataifa mengine yanaweza kufuata mkondo huo hivi karibuni.

"Nadhani ni muhimu kwamba hatua hii imekuja wakati ambapo tunakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu Gaza, na nadhani utambuzi huu unatokana na kile Israeli inachofanya kuliko ambacho Palestina imefanya kufanikisha utambuzi huu katika hali ya sasa," alisema Istrefi.

Mipango hiyo ilizinduliwa wiki iliyopita na mawaziri wakuu wa nchi hizo tatu, na kusababisha ghadhabu nchini Israeli na kuzidisha mvutano wake wa kidiplomasia, hasa na Uhispania.

Soma pia: Wapalestina waadhimisha kumbukumbu ya miaka 76 ya Nakba

Wiki iliyopita, naibu wa Sanchez kutoka mrengo mkali wa kushoto Yolanda Diaz alipongeza hatua hiyo akisema: "Hatuwezi kuacha. Palestina itakuwa huru kutoka mtoni hadi baharini", kauli ambayo balozi wa Israel nchini Uhispania aliilaani na kuitaja kuwa wito wa wazi wa kufutwa kwa Israel.

Mgawiko miongoni mwa mataifa ya magharibi

Kutambuliwa kwa taifa la Palestina kumeibua mabishano makali miongoni mwa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Kwa miongo kadhaa, kutambuliwa rasmi kwa taifa la Palestina kumeonekana kama hatua ya mwisho wa mazungumzo ya amani kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Vita ya Gaza- Rafah
Vita vya sasa vya Gaza vimeongeza msukumo wa kutaka kuundwa kwa taifa la Palestina.Picha: Jehad Alshrafi/AP/dpa/picture alliance

Marekani na mataifa mengi ya Ulaya Magharibi yamesema yapo tayari siku moja kutambua taifa la Palestina, lakini si kabla ya makubaliano kuhusu masuala nyeti kama vile hadhi ya Jerusalem na mipaka ya mwisho. Umwagaji damu unaoendelea Gaza umefufua wito kwa Wapalestina kupewa taifa lao.

Hatua ya Jumanne itamaanisha mataifa 145 kati ya 193 ya Umoja wa Mataifa sasa yanatambua taifa la Palestina.

Mwaka 2014, Sweden ilikuwa mwanachama wa kwanza wa Umoja wa Ulaya kutambua taifa la Palestina, ikifuata mataifa mengine sita ya Ulaya yaliochukuwa hatua hiyo kabla ya kujiunga kanda hiyo, Bulgaria, Cyprus, Jamhuri ya Czech, Hungary, Poland na Romania.

Soma pia: Baraza Kuu la UN laidhinisha ombi la uanachama wa Palestina

Mnamo Oktoba 7, wapiganaji wa Hamas walivamia kusini mwa Israel katika shambulio lililoua zaidi ya watu 1,170, wengi wao wakiwa raia, kulingana na takwimu rasmi za Israeli. Wanamgambo hao pia walichukua mateka 252, ambapo 121 kati yao wanasalia Gaza. Israel inasema 37 kati yao wamekufa.

Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yameua zaidi ya watu 36,000 huko Gaza, pia wengi wao wakiwa raia, kulingana na wizara ya afya ya eneo linalosimamiwa na Hamas.

Chanzo: Mashirika