Uchumi wa Ujerumani mkabala na mitihani ya kimataifa | Masuala ya Jamii | DW | 08.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Uchumi wa Ujerumani mkabala na mitihani ya kimataifa

Matumaini yangaliko bado juu ya uchumi wa Ujerumani

Biashara ya rejareja katika maduka ya mjini Kolon, Ujerumani

Biashara ya rejareja katika maduka ya mjini Kolon, Ujerumani

Kuengezeka uzalishaji wa bidhaa viwandani hapa Ujerumani na kusafirishwa njee bidhaa hizo, kutokana na takwimu zilizokusanywa hivi karibuni, kumesaidia kuengeza matumaini kwamba uchumi wa nchi hii, ulio mkubwa kabisa hapa Ulaya, huenda ukaweza kuepuka mtikiso wa kudidima chini mwaka huu. Wakati uzalishaji viwandani umepanda kwa wastani katika mwezi wa Juni, mazao makubwa ya Ujerumani yanayosafirishwa ngambo yameongezeka sana wakati huo kwa kiwango cha asilimia 4.2, licha ya wasiwasi unaozidi kuweko kuhusu hali ya uchumi.

Wakati fulani wanauchumi wengi waliona kama kitu kinachoisaidia Ujerumani kuweza kuhimili misukosuko ya sasa ya uchumi duniani, matumizi ya watu binafsi nchini yamepungua sana kutokana na kupanda sana bei za nishati zilizousukuma ughali wa maisha kufikia kipimo kisichowahi kuonekana katika miaka ya karibuni na uchumi kuonesha sura ya kupwaya.

Imani ya wateja hapa Ujerumani imepungua na imefikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kuonekana mnamo miaka mitano iliopita, na biashara ya rejareja ilipungua sana mwezi Juni.

Matthias Rubisch, mwanauchumi wa Benki ya Commerz hapa Ujerumani, amesema uchumi katika nchi nyingine za Ulaya Magharibi unapungua sana kwa kasi, na karibu nchi zote kubwa za Ulaya Magharibi zimeshafikia au karibu ziko katika ukingo wa uchumi wao kwenda chini. Na ilivyokuwa Ujerumani inategemea sana kuuza bidhaa zake ngambo, hiyo ina maana haitaweza kuiepuka hali hiyo.

Tarakimu zitakazotolewa wiki ijayo zinatarajiwa kuonesha kwamba kupanda uchumi wa Ujerumani kutapungua katika robo ya pili ya mwaka huu, wakati mnamo robo ya kwanza ya mwaka huu ulipanda juu sana, hali ambayo haijawahi kuonekana katika miaka 12 iliopita. Afisa mmoja wa serekali alinukuliwa akisema kwamba uchumi utakwenda chini kwa asilimia moja katika robo ya pili ya mwaka huu, ukilinganisha na kupanda kwa asilimia 1.5 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Kwenda juu uchumi katika mwezi wa Juni kumetokana na ziyada ya usafirishaji bidhaa kwenda ngambo katika mwezi huo, bidhaa zilizofikia thamani ya Euro bilioni 19.7. Nyongeza katika bidhaa za kwenda ngambo ilifikia asilimia 7.9. Maombi ya bidhaa zilizosafirishwa hadi nchi za Umoja wa Ulaya yalipanda kwa asilimia 12, huku maombi ya kutaka bidhaa zipelekwe Asia, Mashariki ya Kati na Ulaya Mashariki yalisaidia kuziba pengo lililoachwa kwa kupungua usafirishaji wa bidhaa hadi Marekani na sehemu nyingine za Ulaya, kama vile Uengereza na Spain. Bidhaa za Ujerumani zilizosafirishwa hadi katika nchi 15 shirika kwenye eneo la sarafu ya Euro zilizidi kwa asilimia 4.7 katika mwezi wa Juni na kwa asilimia 5.9 kuelekea nchi 27 za Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo, tarakimu zilionesha Ujerumani ilipunguza kuagizia bidhaa kutoka ngambo kwa asilimia moja.
 • Tarehe 08.08.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Et2C
 • Tarehe 08.08.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Et2C
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com