1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Tume ya Chande yawasilisha ripoti yake kwa Rais Samia

23 Aprili 2026

Tume huru ya uchunguzi wa vurugu za wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 Tanzania, imekabidhi ripoti yake mbele ya rais wa taifa hilo Samia Suluhu Hassan, viongozi wa serikali, kikanda na kimataifa.

https://p.dw.com/p/5Ci7x
Tansania 2026 | Mohamed Chande Othman & Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: Tanzania state House 

Ripoti hiyo imebaini kuwa watu 518 walipoteza maisha, wanaume wakiwa 490, wanawake 28 na watoto 21 huku ripoti hiyo ikitaja vyanzo na vichocheo vya vurugu hizo. Taarifa zinaonesha kuwa vifo hivi havikuwa vya kawaida wala halali. Kwa mgawanyo wa kijiografia, Dar es Salaam iliongoza kwa vifo 182, ikifuatiwa na Mwanza 90, Mbeya 80 na Arusha 53.

Hatimaye siku 153 zilizosubiriwa kwa shauku kubwa na watanzania, Afrika na ulimwengu mzima leo zimetimia baada ya tume huru ya uchunguzi wa vurugu za oktoba 29 wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania, kuwasilisha ripoti yake kamili leo.

Mwenyekiti wa tume hiyo,Jaji Mstaafu, Mohamed Othman Chande, alianza kuisoma ripoti hiyo mnamo saa 5 na dakika 14 asubuhi katika Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam.

 Mbele ya Rais, viongozi mbalimbali kutoka ukanda wa Afrika ripoti ya Jaji Chande, ilibaini kuwa watu 518 walipoteza maisha kutokana na vurugu hizo na Ushahidi ukionyesha baadhi ya vifo hivyo vilihusisha matumizi ya risasi na vitu vyenye ncha kali.

"Kadhalika ripoti hiyo  ilibainisha kuwa vyanzo vitano na vichocheo 8 vilivyosababisha vurugu hizo."

Ripoti ilibaini matukio ya watu kutekwa

Baadhi  ni masuala ya kisiasa yanayohusu hitaji la Katiba mpya, uimarishaji wa demokrasia ya vyama vingi, pamoja na madai ya maboresho ya tume huru ya uchaguzi. Pili, ni masuala ya kiuchumi na kijamii yanayogusa ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira na masuala ya kiutawala yanayohusisha mmomonyoko wa maadili,

Ripoti hiyo kadhalika imebaini kuwa Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, jumla ya watu 758 waliripotiwa kutekwa au kupotea, ambapo 113 walipatikana, huku 445 wakiwa bado hawajapatikana.

"Ripoti imebaini kuwa Vifo 502 (asilimia 96.9) vilihusisha raia, huku vifo 16 (asilimia 3.1) vikihusisha maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama."

Aidha, tume ilipokea mawasilisho ya maandishi 323 pamoja na 527 yaliyowasilishwa kwa njia ya maandishi. Tume pia ilifanya ziara muhimu mikoani, ambapo ilikutana na kujadiliana na vikundi 170 vyenye jumla ya washiriki 2,079. Katika jiji la Dar es Salaam, tume ilikutana na washiriki 1,436 kutoka makundi mbalimbali.