Waziri Gabby Bugaga apatikana amekufa Burundi
16 Aprili 2026
Kwa muda mfupi wa majukumu yake ya uwaziri, Gabby alionekana kufuatilia kwa karibu uandishi habari na kuboresha kazi za mitandao ya kijamii husuan Yuotube. Ni hayati Gabby Bugaga katika mahojiano na DW muda mfupi baada ya kuteuliwa kuwa waziri wa habari na ufundi wa kisasa wa mawasiliano.
Mwili wake waziri Gabby Bugaga umeonekana ndani ya gari lake la kiwaziri asubuhi ya leo katika eneo la tabarare la Kivoga umbali wa kilometa 20 kaskazimi mwa Bujumbura, eneo kunakolimwa vigasi.
Gari lake hilo limeonekana kuharibika sehemu ya nyuma na sehemu ndogo ya upande wa kushoto kuliko na usukani huku mwili wake waziri ukiwa umeinamia sehemu ya kulia. Hata hivyo hakujaonekana gari alilogongana nalo ama kilichosababisha ajali hiyo. Hali iliyozusha duku duku juu ya sababu za kifo chake.
Kifo cha Bugaga chaacha simanzi kubwa Burundi
Ni kwenye majira ya saa 2 unusu ndipo timu ya mawaziri yule wa mambo ya ndani na usalama, waziri wa sheria pamoja na katibu mkuu aliye pia msemaji wa serikali walipowasili eneo la tukio na hatimaye maiti yake Gabby Bugaga kuondolea.
Kifo chake Gabby Bugaga waziri wa habari Burundi kimeacha simanzi kubwa katika ulimwengu wa waandishi habari nchini ambapo kwa muda mfupi amekalia kiti cha uwaziri Gabby Bugaga alionekeana kuboresha mengi katika sekta hiyo.
Mousses Habyarimana aliyefanya naye kazi kwenye kituo cha Redio na Televisheni ya taifa, anasema Gabby ameliacha pengo kubwa kwani alikuwa akiitambuwa kazi ya uandishi na kujaribu kuiboresha.
Kwa upande wake Haidallah Hakizimana muandishi pia wa habari anasema waziri Gabby Bugaga ameliacha pengo ambalo itakuwa vigumu kuliziba.
Hadi wakati huu nikiripoti bado hakujatolewa tamko rasmi la serikali kuhusiana na kifo cha waziri wake wa habari na ufundi wa kisasa wa mawasiliano.