1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump kushtakiwa kufuatia malipo kwa Stormy Daniels

John Juma
31 Machi 2023

Baraza kuu la mahakama ya New York limeidhinisha rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ashtakiwe.

https://p.dw.com/p/4PXgE
USA I Donald Trump hält die erste Kundgebung des Präsidentschaftswahlkampfes 2024 in Texas ab
Picha: Nathan Howard/AP/picture alliance

Mashtaka dhidi ya Trump yanatokana na uchunguzi dhidi ya madai kwamba alimlipa muigizaji wa filamu za ngono Stormy Daniels ili anyamaze na kutofichua kuhusu madai ya mahusiano ya kimapenzi kati yao. 

Hatua hiyo inamfanya Donald Trump mwenye umri wa miaka 76, kuwa rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kushtakiwa kwa makosa ya jinai.

Mashtaka yanayohusiana na malipo yaliyofanywa kwa niaba yake mnamo mwaka 2016 wakati wa kampeni zake kuwania urais.

Usalama waimarishwa mjini New York

Mashtaka hayo yanajiri mnamo wakati mwanasiasa huyo Mrepublican akikabiliwa na chunguzi nyingine za kisheria dhidi yake, na vilevile mnamo wakati amezindua kampeni za kutaka kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2024.

Trump pamoja na wafuasi wake wanadai kuwa masaibu yanayomkabili kisheria ni hujuma za kisiasa.
Trump pamoja na wafuasi wake wanadai kuwa masaibu yanayomkabili kisheria ni hujuma za kisiasa.Picha: Brandon Bell/AFP/Getty Images

Uchunguzi umekuwa ukifanywa kwa wiki kadhaa dhidi ya Trump kuhusu madai kwamba alimlipa nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels, kima cha dola 130,000 ili awe kimya kuhusu tuhuma zake kwamba aliwahi kushiriki ngono na mwanasiasa huyo miaka ya nyuma.

Mashtaka hayo yatakuwa mtihani kwa chama cha Republic ambacho tayari kimegawika, kama kimuunge mkono Trump katika uchaguzi ujao au la.

Kwa sehemu mgawanyiko huo unasababishwa na zilizokuwa juhudi za Trump kuuhujumu ushindi dhidi yake katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Kamati ya Bunge la Marekani yatoa ripoti ya uvamizi wa Januari 6

Trump ameyakana madai dhidi yake na anawashutumu waendesha mashtaka kwa kile anachosema ni ‘kumuandama kisiasa' ili kuhujumu kampeni zake.

Wakili wa Trump Joe Tacopina amesema rais huyo wa zamani hakufanya hatia yoyote na ameapa kupambana vikali mahakamani dhidi ya kile alichokitaja kuwa mashtaka ya kisiasa.

Donald Trump akiwa katika mkutano wa kisiasa Texas mnamo Machi 25, 2023.
Donald Trump akiwa katika mkutano wa kisiasa Texas mnamo Machi 25, 2023.Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa wilaya ya Manhattan Alvin Bragg, imethibitisha kwamba imewasiliana na mawakili wa Trump usiku wa Alhamisi ili kuweka utaratibu wa kujisalimisha kwa Trump kwa maafisa wa usalama mjini New York.

Mnamo Machi 18, Trump alitangaza kwamba alitarajia kukamatwa kuhusu malipo kwa Daniels. Trump pia aliitisha maandamano huku akitahadharisha kwamba nchi hiyo inaweza kukumbwa na "vurugu na maafa”.

Wakili wa zamani wa Trump Michael Cohen ambaye tayari alishatoa ushuhuda mbele ya baraza kuu la mahakama, aliliambia bunge mnamo 2019 kwamba alitoa malipo kwa Daniels kwa niaba ya Trump. Na baadaye alirejeshewa fedha hizo.

Uamuzi kuhusu uchunguzi huo wa New York ndio wa kwanza kati ya chunguzi tatu kuu dhidi ya Trump.

Vyanzo: APE, AFPE