Trump awasilisha hoja ya uwezekano wa kushambulia Iran
25 Februari 2026
Trump amesema Iran inatengeneza makombora yanayoweza hata kushambulia Marekani lakini hataruhusu Iran akiitaja kama mfadhili mkubwa zaidi wa ugaidi duniani kumiliki silaha ya nyuklia.
Katika hotuba yake, Trump alielekeza lawama kwa matendo ya Iran ikiwemo kuunga mkono makundi yenye misimamo mikali, mauaji ya waandamanaji, pamoja na programu za nchi hiyo za makombora na nyuklia kama vitisho kwa eneo hilo na kwa Marekani.
Madai ya Trump dhidi ya Tehran yanajiri mnamo wakati amerundika zana za kivita na jeshi kubwa huko Mashariki ya Kati karibu na Iran. Lakini hapo awali hakuwa ametoa maelezo mengi kuwaeleza wananchi wa Marekani kwa nini anaweza kuanzisha vita kali na Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Kwenye hotuba yake ya zaidi ya saa moja na dakika 45 mbele ya mabaraza ya bunge la Marekani, Trump alihoji kuwa, utawala wa Iran na washirika wake wameeneza ugaidi, vifo na chuki. Na kwamba kwa sasa Iran imeanzisha tena programu yake ya nyuklia kwa lengo la kutengeneza makombora ambayo hivi karibuni yatakuwa na uwezo wa kufika Marekani.
Isitoshe Trump amedai kuwa taifa hilo linahusika na mashambulizi ya mabomu ya kutegwa barabarani ambayo yameua wanajeshi wa Marekani na raia.
"Chaguo langu ni kutatua tatizo hili kupitia njia za kidiplomasia. Lakini jambo moja ni hakika: sitaruhusu kamwe mfadhili namba moja wa ugaidi duniani, ambaye bila shaka ndio wao, kumiliki silaha ya nyuklia. Hatuwezi kuruhusu hilo litokee,” amesema Trump.
Iran yataja madai ya Trump kuwa Uwongo Mkubwa
Iran tayari imekanusha madai ya Trump. Kupitia ukursa wa X, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baqaei ameandika kuwa madai ya Trump kuhusu mpango wake wa nyuklia ni marudio ya uwongo mkubwa.
Mapema mwezi huu, waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema kwenye mahojiano yake na kituo cha televisheni Al-Jazeera kwamba Tehran haina uwezo wa kushambulia ndani ya Marekani, lakini itashambulia kambi za kijeshi za Marekani zilizoko Mashariki ya Kati ikiwa Washington itaishambulia.
Hotuba ya Trump kuhusu hali ya taifa pia iligusia masuala kadhaa ikiwemo uhamiaji, ushuru wa bidhaa za kimataifa, hali ya Uchumi na siasa za ndani.
Hotuba ya Trump yatoa dira ya Marekani
Hotuba hiyo imepewa uzito mkubwa na vyombo vya habari sio tu ndani ya Marekani bali kimataifa kwa sababu, inatoa dira ya Washington kisiasa na pia kuonyesha namna utawala wa Trump ulivyojipanga kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa hilo.
Kuhusu ushuru, Trump alisema uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu ushuru ni ‘wa kusikitisha'.
Kuhusu sera ya uhamiaji, alitetea msimamo wake mkali akisema ni wajibu wa serikali ya Marekani kulinda raia wa Marekani na si wageni waliofika kinyume cha sheria.
Trump vilevile alijimwagia sifa akidai kuwa Marekani imeimarika zaidi, ni tajiri zaidi na ni imara zaidi kuliko hapo awali tangu alipochukua hatamu za urais kwa muhula wake wa pili Januari 2025.
(DPAE; AFPE, EBU)