1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Kuna nafasi nzuri ya amani kwa mazungumzo ya Ukraine

1 Desemba 2025

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa ana matumaini baada ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa Ukraine na serikali yake kuhusu njia za kumaliza vita vya Ukraine.

https://p.dw.com/p/54Wl8
Marekani, Washington D.C. 2025 | Donald Trump anazungumza na walinzi wa kitaifa na polisi
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Jacquelyn Martin/AP Photo/picture alliance

Akizungumza ndani ya ndege ya Air Force One, aliielezea Ukraine kuwa na ‘matatizo madogo magumu' na kusema kashfa ya ufisadi nchini humo ‘haiwezi kusaidia.' Trump hakujibu swali la mwandishi iwapo suala hilo litakwamisha mazungumzo ya amani, na muda mfupi baadaye akasema: ‘Nadhani kuna nafasi nzuri ya kufikia makubaliano.' Kwa mara nyingine, Trump alisisitiza imani yake kwamba Urusi na Ukraine zote zinataka kumaliza vita. Rais huyo wa Marekani alithibitisha kuwa mjumbe wake maalum, Steve Witkoff, atakutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow wiki ijayo, ingawa hakutaja tarehe kamili ya kikao hicho. Mapema Jumapili, Witkoff, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio na maafisa wengine wa serikali ya Marekani walikutana na ujumbe wa Ukraine katika jimbo la Florida kujadili mpango uwezekanao wa amani.