1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump apigia turufu maazimio ya mauazo ya silaha

Amina Mjahid
25 Julai 2019

Rais wa Marekani Donald Trump ameyapigia turufu maazimio matatu yaliyonuiwa kuizuwia serikali yake kuiuzia Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu - UAE - silaha za mabilioni ya fedha.

https://p.dw.com/p/3MjXd
USA Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Balce Ceneta

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo mwezi uliopita alizungumzia kitisho kutoka Iran kama sababu ya bunge kuidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 8.1 kwa washirika hao wawili wa Marekani katika Ghuba ya uajemi.

Saudi Arabia ndiyo hasimu mkuu wa Iran, na hali ya wasiwasi imeongezeka kati ya Iran na Umoja wa falme za kiarabu  juu ya masuala tofauti ikiwemo ushirikiano wa UAE na Marekani  katika mikakati ya kuzuwiya kile ilichokiita vitendo vya uchokozi katika kanda.

USA 2019 Trafficking in Persons report | Mike Pompeo, Außenminister in Washington
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike PompeoPicha: Reuters/Y. Gripas

Katika barua aliyoiandika kwa Baraza la Senate kuelezea sababu ya kupinga maazimio hayo, Trump alisema  yataidhoofisha Marekani kiushindani duniani na kuharibu mahusiano muhimu iliyonayo na washirika wake.

Ikulu ya Marekani ilisema kusimamisha mauzo hayo, kutatoa  picha kuwa Marekani haiko pamoja na washirika wake wakati ambapo vitisho dhidi yao vinaongezeka.

Mauzo ya silaha yanayogharimu dola bilioni 8 yanajumuisha silaha za kijeshi, mabomu, risasi  na msaada wa kutengeneza ndege kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Wabunge waungana kupitisha azimio la kuzuwiya mauzo ya silaha

Uamuzi wa mwezi Mei wa Rais huyo wa Marekani Donald Trump kuuza silaha hizo kwa njia ambayo ingelikwepa uidhinishwaji wa bunge iliwakasirisha wabunge, na kuchuku hatua ya pamoja ya wabunge wa Democrats na wale wa Republican ya kupitisha azimio la kuziwiya mauzo ya silaha.

USA Mueller Bericht l  Justizausschuss des Senats l Parlamentspräsidentin Nancy Pelosi
Spika wa baraza la wawakilishi nchini Marekani Nancy Pelosi Picha: Reuters/Y. Gripas

Hasira zimekuwa zikishuhudiwa katika bunge la Congress kufuatia utawala wa Trump kuwa na mahusiano ya karibu na Saudi Arabia inayojihusisha na vita vya Yemen vilivyosababisha mauaji ya raia wasiokuwa na hatia katika operesheni ambayo Marekani inaisasdia.

Hasira pia ziliongezeka kutokana na mauaji ya mwandishi habari raia wa Saudi Arabia aliyeishi Marekani Jamal Khashoggi na yanayodaiwa kufanywa na maafisa wa Saudi Arabia.

Katika taarifa yake spika wa baraza la wawakilishi nchini Marekani Nancy Pelosi amesema hatua ya rais Trump kutumia kura ya turufu kupinga maazimio inapuuza uamuzi usio wakivyama na uliyoungwa mkono na mabaraza yote ya bunge na kuendeleza utawala wake kujihusisha na vita vya Yemen jambo linalomtia doa rais huyo.

Vyanzo: afp/Reuters/dpa