THE HOPE FOR CHANGES IN CUBA ONE MONTH SINCE RAUL TOOK OVER | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

THE HOPE FOR CHANGES IN CUBA ONE MONTH SINCE RAUL TOOK OVER

Nchini Cuba hivi sasa wadadisi, wanasiasa na wananchi kwa ujumla wanajiuliza ni kipi kinachopikwa katika jiko la siasa za nchi hiyo?

Rais Raul Catro wa Cuba

Rais Raul Catro wa Cuba


Hata hivyo mwezi mmoja toka Raul Castro ashike hatamu kamili ya urais wa nchi hiyo, bado menyu au orodha ya mabadiliko yanayotayarishwa haijatoka, ingwaje harufu ya mwanzo imeanza kusikika.


Uvumi pamoja na matamshi yanayotolewa na vyombo vya habari vya serikali, vinaashiria kuwepo kwa uwezekano wa mabadiliko ikiwemo uhuru wa kuuza bidhaa za mazao, computer na vifaa vya majumbani.


Pia taarifa za kulegezwa kwa sheria za uhamiaji ni ishara ya kuwepo kwa mabadiliko hayo, ingawaje hata hivyo hakuna taarifa rasmi za serikali juu ya hatua hizo.


Rais Raul Castro ambaye ni mdogo wake na Kiongozi wa nchi hiyo aliyestaafu, Fidel Castro, mwenyewe wakati wa hotuba yake mwezi uliyopita alionesha kuhamasisha matumaini ya kuwepo kwa mabadiliko katika uongozi wake.


Katika hotuba hiyo Raul alisema kuwa ataondoa baadhi ya marufuku na sheria katika kipindi cha wiki chache na kupambana na matatizo mengine kama vile kushuka kwa thamani ya sarafu na kufanya mabadiliko ya kiuchumi.


Afisa mmoja wa ngazi ya juu nchini humo hivi karibuni alisema kuwa serikali hiyo hivi sasa inatafakari jinsi ya kuondoa vikwazo vyote ambavyo vinawazuia wananchi kuishi maisha ya kawaida.Hata hivyo hakufafanua zaidi.


Lakini wadadisi wa siasa za Cuba wanasema kuwa mwezi mmoja wa Raul kuwepo madarakani baada ya miongo kadhaa ya utawala wa Fidel Castro, kitu pekee kilicho wazi ni kwamba mabadiliko yoyote yatakayofanywa hayatatangazwa na viongozi wa juu wa serikali.


Wanasema kuwa uwezekano ni kwamba mabadiliko hayo yatafanyika taratibu na kwa tahadhari, kama vile wakulima kuuziwa zana za kilimo hatua ambayo tayari imekwishaanza kuchukuliwa katika baadhi ya majimbo kufuatia tangazo tu la kwenye radio ya taifa.


Lakini mchumi mmoja wa nchi hiyo Oscar Espinosa Chepe ameonya kuwa usiri huo hautarahisisha mambo na kwamba hiyo ndiyo tabia ya Rais Raul Castro ya kupenda kufanya kazi kwa siri.


Amesema kuwa hatari iliyopo kwa utaratibu huo wa mabadiliko ya siri ni kwamba unaweza kufika wakati serikali ikaamua kurejea katika mfumo wa zamani kwa hiyo mabadiliko hayo hayana uhakika.


Mwanadiplomasia mmoja wa nchi za Ulaya aliyeko nchini Cuba alisema kuwa kuna vuguvugu la chini kwa chini la mabadiliko ya kisera nchini humo.Hata Marekani imekiri kuwepo kwa mbinu hizo za mabadiliko zinazochukuliwa na Raul Castro.


Shahuku ya mabadiliko ya kisera na kiuchumi ni kubwa miongoni mwa wananchi wa Cuba kitu ambacho hata vyombo vya habari vya serikali vimekuwa vikiyakinisha.


Lazzaro Barredo ambaye ni mhariri mkuu wa gazeti la Granma amesema kuwa ana wasi wasi anapoangalia jinsi wananchi walivyo na matumaini ya kwamba kutangazwa kwa mabadiliko hayo kutatatua matatizo yanayowakabili katika muda mfupi.


Shirika la habari la Cuba AIN lililazimika kukanusha uvumi wa kupanda kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo PESO ukihusishwa na hisia zilizopo.


Kwa mchumi Espinosa Chepe kuna hisia zinazochomoza nchini humo katika sekta zote ikiwemo ndani ya chama chenyewe tawala cha kikomunisti cha PCC.


Mwezi huo mmoja ukiingiza Cuba katika zama mpya, ladha ya mabadiliko huenda ikawa tayari na ni dhahiri kuna njaa ya mabadiliko.Hata hivyo ni kusubiri ni kwa kiwango gani menu au orodha ya mabadiliko hayo itakuwa.

 • Tarehe 25.03.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DTms
 • Tarehe 25.03.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DTms
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com