Sudan: Jeshi laingilia kuwanusuru waandamanaji | Matukio ya Afrika | DW | 08.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Sudan

Sudan: Jeshi laingilia kuwanusuru waandamanaji

Hatua ya wanajeshi wa Sudan ni kwa ajili ya kuwalinda waandamanaji baada ya vikosi vya usalama kujaribu kuwaondoa maelfu ya waandamanaji walioweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi katikati ya mji mkuu, Khartoum.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir amepinga wito wa maalfu ya wananchi wake wanaomtaka ang'atuke. Katika muktadha wa kuongezeka shinikizo dhidi ya utawala wa rais huyo wananchi wanalitaka jeshi liingilie kati na limtoe madarakani kwa nguvu. Waandamanaji hao wala hawakujali kufyatuliwa mabomu ya kutoa machozi bali waliendelea kupaza sauti zao. Wakati huo huo wanalitaka jeshi liwaunge mkono katika harakati yao.

Tangu maandamano hayo yalipoanza kote nchini Sudan mnamo mwezi Desemba maafisa wa idara ya usalama wa taifa, wale wa idara ya Upelelezi na polisi wameendelea kuwakamata watu wanaoandamana lakini jeshi halikuwahi kuingilia kati. Waandamanaji tangu siku ya Jumamosi wamekita kambi karibu na makao makuu ya jeshi ambako pia ni makao ya Rais al- Bashir pamoja na Wizara ya Ulinzi. Maandamano hayo makubwa ya kupinga serikali yameendelea kwa miezi kadhaa sasa.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir (Reuters/M. Nureldin Abdallah)

Rais wa Sudan Omar al-Bashir

Kwa mujibu wa taarifa za shirika la habari la AFP askari wameweka vizuizi barabarani karibu na eneo hilo baada ya kushindwa kuwaondosha waandamanaji. Waandaaji wa maandamano hayo wamewataka wakazi wa Khartoum na maeneo ya karibu wajiunge na waandamanaji wengine ambao wamejitokeza mabarabarani kwa siku tatu mfululizo.

Kwenye taarifa yake chama cha waandaaji hao kinachoitwa Alliance for Freedom and Change kimevilaumu vikosi vya usalama vya serikali kwa kujaribu kuwaondoa waandamanji hao kwa kutumia nguvu. Mkusanyiko huo wa watu wengi nje ya makao makuu ya jeshi ni kubwa zaidi tangu maandamano yalipoanza katika mji wa kati wa Atbara, mnamo Desemba 19 na kuenea haraka hadi kwenye mji mkuu, Khartoum na miji mingine nchini Sudan kote.

Idara ya mambo ya nje ya Umoja wa Ulaya imesema ni dhahiri idadi kubwa ya watu inataka mabadiliko baada ya kukabiliwa na vikwazo kwa miaka mingi na kwamba serikali inapaswa kuyashughulikia madai yao kwa kuchukua hatua zifaazo.

Waandamanaji wanaulalamikia utawala wa rais Omar al-Bashir kwa usimamizi mbaya wa uchumi jambo ambalo limesababisha bei za vyakula kuongezeka pamoja na uhaba wa mara kwa mara wa mafuta na fedha za kigeni. Serikali inakanusha madai hayo na badala yake inalaumu vikwazo vya Marekani kwa kusababisha matatizo ya kiuchumi nchini Sudan.

Vyanzo: AFP/RTRE