1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steimeier awataka Wajerumani kuilinda demokrasia

Mohammed Khelef
24 Desemba 2019

Miaka 30 baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, Wajerumani wanapaswa kuyakumbuka maadili ya kidemokrasia yaliyowaunganisha, anasema Rais Frank-Walter Steinmeier kwenye hotuba yake ya kila mwaka ya Krismasi kwa taifa. 

https://p.dw.com/p/3VIYt
!!! SPERRFRIST BEACHTEN !!! - Berlin | Fototermin zur Weihnachtsansprache des Bundespräsidenten Frank-Walter Steinmeier
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Mwaka 2019 ulishuhudia kutimia miaka 30 tangu vuguvugu la kidemokrasia kutoka ngazi za chini kabisa kufanikiwa kuuangusha Ukuta wa Berlin na utawala wa kindamizaji wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki uliokuwa umeujenga ukuta huo.

Lakini pia ni mwaka ambao ulimshuhudia mfuasi mmoja wa siasa kali za kibaguzi akiwauwa watu wawili kwenye mji wa mashariki wa Halle, baada ya kushindwa kuingia kwenye sinagogi alikodhamiria kufanya mauaji makubwa katika sikukuu ya Mayahudi ya Yom Kippur.

Wakati mikasa kama hiyo ikiiandama jamii ya Kijerumani, Rais Steimeier alitumia hotuba yake ya kila mwaka ya Krismasi kuwataka Wajerumani kuikumbatia mijadala hata iliyo mikali lakini kamwe wasikubali kuchukuliwa na hisia kali za kibaguzi na chuki dhidi ya Mayahudi ambazo zinahujumu maendeleo ya kidemokrasia yaliyopatikana ndani ya miongo mitatu iliyopita.

"Tunaihitajia demokrasia - lakini kwa sasa demokrasia inatuhitajia sisi," alisema kwenye hotuba hiyo akiwa katika Kasri la Bellevue mjini Berlin, akiongeza kwamba "demokrasia inawahitaji raia wanaojiamini ambao wana imani na dhamira, maarifa na hehsima, na ambao wanaonesha mshikamano na wengine."

'Demokrasia iko nasi'

Gemeindetag des Zentralrats der Juden in Deutschland
Rais Steinmeier akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Mayahudi nchini Ujerumani tarehe 19 Disemba 2019.Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kwenye hotuba ya mwaka jana, Rais Steinmeier aliwaomba Wajerumani kuangalia zaidi yale yanaowaunganisha na wale wenye mitazamo tafauti na wao. Mwaka huu, anahoji ni jinsi gani Wajerumani walio kwenye kipindi kilichotandwa na siasa wanaweza "kujifunza kuheshimiana licha ya mpasuko mkubwa uliopo."

"Vipi tunaweza kuhakikisha kwamba mijadala yetu inakuwa ya kujenga zaidi na sio yenye sauti za kutisha? Vipi tunaweza kujenga mualaka munamo tafauti nyingi zilizopo? Je, tuna mambo machache zaidi yanayotuunganisha kuliko yanayotugawa?" Aliuliza kwenye hotuba yake hiyo.

Rais Steinmeier aligusia mashambulizi mjini Halle kwenye sinagogi la Mayahudi wakati akijaribu kuyajibu maswali ambayo aliyauliza kwenye hotuba yake. Mlango wa sinagogi hilo uliotengenezwa kwa chuma na mbao ndicho kitu pekee kilichomzuwia mshambuliaji huyo aliyekuwa amejihami kwa silaha nzito kuingia na kufanya mauaji makubwa na kuyaonesha moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.

"Mlango huu madhubuti, kwa maoni yangu, unaashiria zaidi ya mlango. Unatuwakilisha sisi," alisema akimaanisha jamii ya Kijerumani. "Lakini je, sisi ni madhubuti? Tunaweza kujilinda? Tunasimama bega kwa bega? Tunalindana?"

'Nyinyi ndio jawabu'

Wakati chuki dhidi ya Mayahudi zikiongezeka nchini Ujerumani, ni wale Wajerumani wanaokabiliana nao michezoni, kwenye vilabu au wanaokabiliana na siasa kali mitandaoni kwa "heshima na adabu", ndio jibu sahihi kwa maswali haya kuhusiana na maadili ya kitaifa kwa mwaka 2019, alisema Steinmeier. "Nyinyi ndio jawabu. Nyinyi nyote!"

Kuakisi juu ya mafanikio ya kidemokraia tangu kuporomoka kwa Ukuta wa Berlin kunaweza kuimarisha nguvu ya raia katika kukabiliana na vitisho vinavyoigawa jamii, aliongeza Steimeier.

Berlin | Basketballspieler Dirk Nowitzki und weitere frewillige erhalten Verdienstorden
Rais Steinmeier akiwa na wafanyakazi wa kujitolea aliowatunuku tuzo ya heshima ya Ujerumani tarehe 4 Disemba 2019.Picha: Reuters/F. Bensch

"Miaka 30 iliyopita, ahadi hii, hamasa hii ya demokrasia, iliwasukuma maelfu ya watu ndani ya Ujerumani Mashariki kuingia mitaani," alisema. "Kwa ujasiri mkubwa mno, mashujaa hawa, majasiri hawa wa kike na kiume, waliauangusha Ukuta chini!"

'Nina imani na nchi hii'

Kwa mujibu wa uchunguzi wa mwezi wa Aprili uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew, asilimia 43 ya Wajerumani wanasema hawaridhishwi na namna demokrasia yao inavyofanya kazi. Hilo ni ongezeko la asilimia 17 kutoka hali ilivyokuwa mwaka 2018, ambalo linatokana na imani kwamba taasisi za Umoja wa Ulaya zinazidi kupoteza umashuhuri wake na ongezeko la jamii za wahamiaji wanaotaka kuwa tafauti kitamaduni na nchi walizohamia, kwa mujibu wa uchunguzi huo.

Lakini Steinmeier alisema ni juu ya Wajerumani kutumia nguvu zao kwenye sanduku la kura kuunda nchi yenye taswira wanayoitaka. Katika chaguzi kadhaa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, Wajerumani wameonesha kuunga mkono chama kinachopingana na mifumo mikongwe na wahamiaji cha AfD au cha watetezi wa mazingira, Green Party.

Hata hivyo, Rais Steinmeier alisema kuwa wito wa kutaka mabadiliko kwenye jamii haupaswi kupotea njia na kuelekea kwenye ukosefu wa heshima, mshikamano na kujitolea kwa ajili ya demokrasia ambayo inawaunganisha Wajerumani wote bila kujali matabaka au misimamo ya kisiasa.

"Najuwa kuwa sifa zote hizi munazo, tunazo ndani yetu, kwenye jamii hii hii," alisema. "Na ndio maana nina imani na nchi hii."