Sierra Leone kuwapokea Waafrika waliofukuzwa kutoka Marekani
16 Mei 2026
Serikali ya Sierra Leone imekubali kupokea mamia ya wahamiaji kutoka Afrika Magharibi wanaofukuzwa kutoka Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje Timothy Kabba amesema makubaliano hayo yatawezesha Sierra Leone kupokea hadi watu mia tatu kwa mwaka kutoka nchi za jumuiya ya Afrika Magraribi ECOWAS, huku kiwango cha juu kwa mwezi kikiwa watu ishirini na watano.
Ndege ya kwanza inatarajiwa kuwasili Mei ishirini ikiwa na wahamiaji ishirini na watano kutoka Senegal, Ghana, Guinea na Nigeria.
Hatua hiyo ni sehemu ya sera ya utawala wa Rais Donald Trump ya kuongeza kasi ya kuwafukuza wahamiaji. Hata hivyo, mashirika ya haki za binadamu na wataalamu wa sheria wameendelea kuhoji uhalali wa kuwapeleka wahamiaji katika nchi ambazo si za uraia wao.
Serikali ya Sierra Leone haijaeleza iwapo wahamiaji hao wataruhusiwa kuishi nchini humo au watarudishwa katika nchi zao za asili.