1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la UNRWA lasitisha usambazaji chakula mjini Rafah

Sylvia Mwehozi
22 Mei 2024

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina UNRWA limetangaza kusitisha usambazaji wa chakula mjini Rafah mnamo wakati ugavi wa misaada ukizidi kupungua na hali ya usalama ikisalia kuwa tete.

https://p.dw.com/p/4g7s4
Rafah | UNRWA
Msaada wa UNRWA RafahPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina UNRWA limetangaza kusitisha usambazaji wa chakula mjini Rafah mnamo wakati ugavi wa misaada ukizidi kupungua na hali ya usalama ikisalia kuwa tete.Ujerumani yalaani ongezeko la ghasia dhidi ya UNRWA

UNRWA imetoa tangazo hilo kupitia mtandao wa X, bila kutoa maelezo zaidi. Shirika jingine la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP, lilionya siku ya Jumanne kwamba operesheni za kiutu katika Ukanda wa Gaza, ziko ukingoni kushindwa.

Umoja wa Mataifa unasema katika muda wa siku mbili zilizopita hakuna msaada wowote ulioingia Gaza kupitia bandari inayoelea iliyojengwa na Marekani. Unapanga kuanzisha njia mpya za kusambaza misaada kutokea kwenye bandari baada ya malori kuzuiliwa na umati wa wakaazi wenye uhitaji.

Usambazaji wa misaada ya kimataifa ulitatizika tangu Israel ilipofunga kivuko cha mpaka cha Rafah kuelekea rasi ya Sinai ya Misri.