1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali, upinzani Syria kuandika katiba mpya

18 Oktoba 2021

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria amesema wenyeviti wenza wa Kamati ya Katiba ya Syria kutoka serikalini na upinzani wamekubaliana juu ya kuandika rasimu ya katiba mpya, hatua muhimu kuelekea kukomesha vita.

https://p.dw.com/p/41pBZ
Geir O. Pedersen, UN-Sondergesandter für Syrien
Picha: Martial Trezzini/picture alliance/KEYSTONE

Mjumbe huyo Maalum wa Umoja wa Mataifa, Geir Pedersen, amesema wenyeviti hao wenza ambao walikutana kwa mara ya kwanza kabla ya mazungumzo ya wiki nzima yanayofanyika mjini Geneva, Uswisi, walikubaliana "kutayarisha na kuanza uandishi wa mabadiliko ya katiba." Aliyaelezea mazungumzo yao kuwa ya ukweli na ya dhati.

Kamati ya kuandika rasimu hiyo yenye wajumbe 45 kutoka serikali, upinzani na asasi za kijamii imepewa jukumu la kupendekeza katiba mpya itakayopelekea hatimaye chaguzi zitakazosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Duru hiyo ya mazungumzo ambayo ni ya sita ndani ya kipindi cha miaka miwili na ya kwanza tangu mwezi Januari kwa kamati ya uandikaji wa katiba, ni muhimu sana kwa mustakabali wa Syria kwani itajadili misingi ya wazi.

"Kamati ya katiba ya Syria ni mchango muhimu kwenye mchakato wa kisiasa, lakini kamati yenyewe pekee haitaweza kuutatuwa mgogoro wa Syria. Kwa hivyo, tunapaswa kushirikiana, kufanya kazi muhimu ya kamati ya katiba, lakini pia kuzungumzia maeneo mengine ya mzozo wa Syria." Alisema Pedersen.

Upinzani wataka usawa uwe sehemu ya katiba

Hadi Al-Bahra, mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Katiba ya Syria akitokea upinzani, alisema ujumbe wa upinzani unataka mageuzi muhimu, yakiwemo haki sawa kwa raia wote wa Syria.

Bashar Assad und Vladimir Putin
Kwa msaada mkubwa wa Urusi, Rais Bashar Al-Assad (kushoto) amefanikiwa kuirejesha sehemu kubwa ya Syria mikononi mwake.Picha: Mikhail Klimentyev/AP/picture alliance

"Kwa kuwa hatuna mgawanyo wa madaraka kwenye katiba ya sasa, kumekuwa na ukosefu wa usawa ambao unatumika kwa njia isiyo sahihi."  Al Bahra alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Ingawa upande wa serikali haukutaka kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mazungmzo hayo, lakini inatazamiwa kuwa kila upande utaleta mapendekezo yao kwa maandishi juu ya mambo yanayohusiana madaraka na utawala wa sheria. 

Vita vya muongo mmoja sasa nchini Syria vilianza na maandamano ya umma dhidi ya utawala wa Rais Bashar Al-Assad mwaka 201.

Baada ya msaada mkubwa wa mshirika wake, Urusi, Assad hatimaye ameweza kurejesha sehemu kubwa ya nchi mikononi mwake, lakini maeneo muhimu bado yanashikiliwa na vikosi vyengine.

Jeshi la Uturuki linashikilia sehemu kubwa ya kaskazini na kaskazini magharibi, huku vikosi vya Marekani vikiwekwa kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi upande wa mashariki na kaskazini mashariki.

Mnamo mwezi Januari, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, Geir Pedersen, alisema wawakilishi wa Assad walikuwa wamekataa mapendekezo ya upinzani na yake yeye kwenye kuupeleka mbele mchakato wa kikatiba, lakini baada ya shinikizo la wanadiplomasia wa Magharibi na wa Urusi, hatimaye kuna matumaini ya uandikaji wa katiba mpya kuanza.