Sanchez kushughulikia matatizo ya Uhispania | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sanchez kushughulikia matatizo ya Uhispania

Waziri Mkuu mteule wa Uhispania, Pedro Sanchez ameapa kushughulikia kwa haraka huduma za kijamii za Wahispania, baada ya miaka kadhaa ya kubana matumizi chini ya serikali ya kihafidhina ya Mariano Rajoy.

Sanchez leo amechukua madaraka baada ya kushinda katika kura ya kutokuwa na imani na Rajoy katika bunge kutokana na madai ya rushwa yanayohusishwa na chama chake cha Popular.

Sanchez amewaambia waandishi habari mjini Madrid kwamba anafahamu kuhusu majukumu ya kisiasa na wakati mgumu ulipo katika nchi hiyo. Kiongozi huyo mpya ameahidi kudumisha maelewano miongoni mwa vyama vya kisiasa ili kuibadilisha Uhispania na kuifanya iwe ya kisasa, pamoja na kushughulikia masuala ya kijamii ya watu wengi ambao wanakabiliwa na hali ya kukosa haki sawa.

''Nitazitatua changamoto zote za nchi yetu kwa unyenyekevu na kujitolea. Nitaibadilisha nchi yetu, jambo ambalo chama chetu cha Kisoshalisti kimekuwa kikifanya tulipokuwa serikalini. Na pili, tutayashughulikia kwa haraka masuala yote ya kijamii ya watu wengi wanaokosa haki,'' alisema Sanchez.

Spanien Madrid - Ministerpräsident Rajoy per Mistrauensvotum gestürzt (Reuters/S. Perez)

Mariano Rajoy

Hata hivyo, uteuzi wa Sanchez mwenye umri wa miaka 46, sasa unahitaji kuchapishwa katika gazeti la serikali kabla ya kuapishwa na Mfalme Felipe wa Sita mapema kesho asubuhi. Baada ya kuapishwa, Sanchez, ambaye hadi sasa ni kiongozi wa chama kikubwa cha upinzani cha PSOE, ataunda baraza la mawaziri katika siku zijazo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Rajoy mwenye umri wa miaka 63, anapaswa kukabidhi barua ya kujizulu kwa mfalme wa Uhispania, kabla mrithi wake hajachukua rasmi madaraka.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, amempongeza Sanchez kwa ushindi huo na amesema umoja huo una imani na serikali mpya ya Uhispania. Juncker amesema ana matumaini nchi hiyo itaendelea kuchangia ili kuufanya umoja huo kuwa imara zaidi na wenye usawa.

Ujerumani imesema itatoa ushirikiano wa uaminifu na kwa karibu kabisa katika serikali mpya ya Uhispania kwa maslahi ya kirafiki ya nchi hizo mbili. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert amesema leo kuwa nchi zote hizo ni wanachama muhimu wa Umoja wa Ulaya. Akizungumza muda mfupi baada ya Rajoy kushindwa katika kura hiyo, Seibert amepongeza mageuzi ya kiuchumi yaliyofanywa na kiongozi huyo anayemaliza muda wake, mshirika wa kihafidhina wa Kansela Angela Merkel.

Brüssel Jean-Claude Juncker; Präsident Europäische Kommission (Getty Images/AFP/J. Thys)

Jean-Claude Juncker

Wakati hayo yakijiri, jimbo la Catalonia leo limetangaza baraza lake jipya la mawaziri hali itakayoifanya serikali kuu ya Uhispania kuacha kuitawala moja kwa moja Catalonia. Baraza hilo lina mawaziri wanane wa kiume na wanawake sita. Serikali ya Catalonia imesema kuwa mawaziri katika utawala wa rais mpya wa jimbo hilo, Quim Torra wataapishwa keho Jumamosi.

Aidha, Torra ametangaza kuwa serikali yake imemfungulia mashtaka Rajoy pamoja na msaidizi wake, Soraya Saenz de Santamaria kutokana na kutumia vibaya madaraka na kulizuia baraza la mawaziri lililopendekezwa awali. Sanchez kwa upande wake amesema ataanza majadiliano na serikali ya Catalonia ili kutafuta ufumbuzi.

Ama kwa upande mwingine, waendesha mashtaka wa Ujerumani leo wametoa maombi mapya kumuweka kizuizini kiongozi wa zamani wa Catalonia, Carles Puigdemont, wakati akisubiri hukumu kuhusu uamuzi wa kurudhishwa Uhispania. Mahakama moja ya kaskazini mwa Ujerumani ilimruhusu Puigdemont kuondoka gerezani kwa dhamana muda mfupi baada ya kukamatwa Machi 25 kutokana na ombi la Uhispania.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Abudl-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com