Rubio asema wanatarajia majibu ya Iran kumaliza mzozo
8 Mei 2026
Rubio amewaambia waandishi habari kuwa wanatumai majibu ya Iran yatawezesha mchakato muhimu wa mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Hata hivyo ameshutumu vikali juhudi za Iran kudhibiti mlango wa Bahari wa Hormuz akisema hazikubaliki. Hayo yamejiri baada ya ripoti kwamba Tehran imeunda mamlaka ya kuamua meli zinazoruhusiwa kupita kwenye njia hiyo muhimu ya Bahari.
"Tumeona ripoti usiku huu kwamba Iran imejaribu kuunda mamlaka itakayosimamia ujia wa kimataifa wa Mlango wa Bahari wa Hormuz. Hilo halitakubalika. Kudhibiti njia ya kimataifa ni kinyume cha sheria na haikubaliki. Dunia inapaswa kuanza kujiuliza itafanya nini ikiwa Iran itajaribu kudhibiti njia ya kimataifa ya baharini,' amesema Rubio
Hapo jana vikosi vya Marekani na Iran vilishambuliana baharini huku Rais Donald Trump akisema makubaliano ya usitishaji vita yangalipo.