1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramadhani yaanza bei za vyakula na nishati zaendelea kupanda

Zainab Aziz Mhariri: Sudi Mnette
2 Aprili 2022

Mwezi mtukufu wa Ramadhan umeanza leo Jumamosi katika baadhi ya nchi huku nchi nyingine zikitarajia kuanza mfungo hapo kesho Jumapili. Upatikanaji wa bidhaa siyo wa kawaida kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/49NPV
Ukraine Krieg -  Folgen für die Nahrungsmittelindustrie Muslime Ramadan Preise Getreide Brot
Picha: FETHI BELAID/AFP

Mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa Waislamu umeanza leo Jumamosi katika sehemu nyingi za Mashariki ya Kati, barani Ulaya na maeneo mengine duniani huku nchi nyingine zikitarajia kuuanza mfungo kesho Jumapili. 

Wengi walikuwa na matumaini ya kuufunga mwezi huu wa Ramadhan kwa furaha hasa baada ya janga la virusi vya corona ambapo Waislamu wapatao bilioni 2 ulimwenguni kote hawakuweza kwenda kuhiji Makka kwa muda wa miaka miwili iliyopita.

Athari za vita vinanvyoendeshwa na Urusi katika mji wa Mariupol nchini Ukraine.
Athari za vita vinanvyoendeshwa na Urusi katika mji wa Mariupol nchini Ukraine.Picha: Sergei Bobylev/TASS/picture alliance/dpa

Wakati huo huo kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mamilioni ya watu katika sehemu mbalimbali duniani wanafadhaika juu ya kupata vyakula hasa kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa ambako kunaathiri zaidi watu ambao wanaishi kwenye maeneo yenye migogoro, kwa mfano katika nchi za Lebanon, Iraq, Syria hadi Sudan na Yemen.

Vita vya nchini Ukraine vimeongeza makali hayo kwa kuwa nchi hiyo pamoja na Urusi zinatoa theluthi moja ya ngano inayotegemewa na nchi kadhaa duniani kuwalisha mamilioni ya watu wake. Urusi na Ukraine pia ni wauzaji wakubwa wa nafaka nyingine pamoja na mafuta ya alizeti yanayotumika kwa kupikia.

Hali ilivyokuwa mjini Mosul, Iraq wakati wa Ramadhan mwaka jana 2021.
Hali ilivyokuwa mjini Mosul, Iraq wakati wa Ramadhan mwaka jana 2021.Picha: Ismael Adnan/SOPA Images/ZUMA Wire/picture alliance

Misri, muagizaji mkuu wa nafaka ya ngano duniani, imepokea sehemu kubwa ya ngano yake kutoka Urusi na Ukraine katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo watu wengi nchini Misri wakati huu wameshindwa kufanya manunuzi makubwa kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kutokana na kukabiliwa na uhaba wa fedha za matumizi wakati ambapo nchi hiyo inakumbwa na hali ngumu kutokana na sarafu yake kushuka thamini sana.

Hali hiyo inaashiria kuwa kwa watu wengi watakuwa na mabadiliko makubwa kwenye kuufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan katika mwaka huu nchini humo na hata kwa wale waliokuwa wakiandaa futari bila malipo mitaani kwa lengo la kuwasiaidia watu masikini.

Mahala pa kuuzia mikate mjini Cairo, Misri
Mahala pa kuuzia mikate mjini Cairo, MisriPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Kupanda kwa bei za vyakula pia kutazidisha matatizo kwa wengi nchini Lebanon ambayo inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, sarafu ya nchi hiyo iliporomoka na kusababisha watu wa tabaka la kati nchini humo kutumbukia katika umaskini.

Akeel Sabah, mwenye umri wa miaka 38, ni muuzaji wa unga wa ngano katika soko la jumla la Jamila la mjini Baghdad nchini Iraq ambaye husambaza bidhaa hiyo kwenye wilaya ya Rasafa iliyo upande wa mashariki wa mto Tigris amesema unga na karibu vyakula vingine vyote vinaagizwa kutoka nje nchini humo. Ameeleza kuwa wauzaji wananunua bidhaa kwa kutumia dola ya Marekani na kwamba zamani tani moja ya unga iligharimu kiasi cha dola 390 lakini sasa ananunua tani hiyo moja kwa dola 625.

Rais wa Misri Abdel Fattah Al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah Al-SisiPicha: Egyptian Presidency/AA/picture alliance

Mfanya biashara huyo Akeel Sabah amesema kushuka kwa thamani ya fedha za Iraq mwaka mmoja uliopita ndio kumesababisha ongezeko la bei za bidhaa na ametahadharisha kuwa mgogoro kati ya Urusi na Ukraine unapoendelea, bei za bidhaa nazo zitaendelea kupanda kwa haraka.

Chanzo:AP