1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Rais Zelensky awarai washirika kuipa Ukraine ndege za kivita

John Juma
8 Februari 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amezihimiza nchi washirika kuipa Ukraine silaha zinazohitajika za kivita ili kuzima uvamizi wa Urusi nchini mwake.

https://p.dw.com/p/4NFJA
Großbritannien | Präsident Wolodymr Selenskyj und Premierminister Rishi Sunak
Picha: Victoria Jones/PA via AP/picture alliance

Amesema hayo wakati wa ziara yake nchini Uingereza. Wabunge wa uingereza walimpongeza Zelensky alipokuwa akiwahutubia wakati wa ziara hiyo ya nadra.

Ziara ya Rais Volodymyr Zelensky Jumatano nchini Uingereza ni ya pili ambayo amefanya nje ya nchi yake tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24 mwaka uliopita. Ziara ya kwanza alifanya Marekani, mwishoni mwa mwaka uliopita.

Akiwahutubia wabunge wa Uingereza, Zelensky aliipongeza nchi hiyo kwa kusimama na taifa lake tangu siku ya kwanza Urusi ilipovamia.

Nchi za Magharibi wameahidi kuipa Ukraine makombora

Alisisitiza umuhimu wa nchi yake kupewa silaha zote muhimu za kivita zikiwemo ndege za kivita ili kuzima uvamizi wa Urusi, kukomboa maeneo yote ambayo Urusi imeyakamata nchini mwake na kusema mwisho wa yote, ushindi utapatikana.

Zelensky: Ushindi wetu utaubadili ulimwengu

"Nina Imani ishara hii itatusaidia katika muungano wetu ujao, muungano wa ndege za kivita na ninawaomba na ulimwengu mzima, kwa maneno mepesi lakini muhimu, muipe Ukraine ndege za kivita, ndege za uhuru,” amesema Zelensky.

Alibeba kofia inayovaliwa na rubani wa kivita wa nchi yake kama zawadi kwa Uingereza. Kofia hiyo iliandikwa ujumbe uliosema, "tuna uhuru, tupe ndege kuulinda uhuru huo".
Alibeba kofia inayovaliwa na rubani wa kivita wa nchi yake kama zawadi kwa Uingereza. Kofia hiyo iliandikwa ujumbe uliosema, "tuna uhuru, tupe ndege kuulinda uhuru huo".Picha: Stefan Rousseau/AP/picture alliance

Ziara ya Zelensky imejiri mnamo wakati nchi yake inapanga kuyakomboa maeneo ambayo vikosi vya Urusi vimekamata, lakini vilevile inajiri wakati Urusi inapanga kuzidisha mashambulizi yake, kuelekea kumbukumbu ya mwaka mmoja wa uvamizi huo.

Zelensky alisema kuwa katika vita vya zamani, uovu ulishindwa hivyo anaamini Urusi itashindwa na kwamba ushindi wao utaubadili ulimwengu.

Zelensky kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Kyiv

Ametaka Urusi kuwekewa vikwazo vikali zaidi kiasi cha kuzima uwezo wowote wa nchi hiyo kufadhili vita hivyo.

Zelensky atarajiwa kuzuru pia Paris na Brussels

Zelensky alisema anazungumza kwa niaba ya raia jasiri wa Ukraine na aliwapongeza Waingereza kwa ujasiri wao wa kusimama nao kidete tangu mwanzo.

Wanajeshi wa kike Ukraine wapata magwanda

Punde alipowasili mjini London, alifanya mkutano na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak

Awali Sunak alitangaza kwamba Uingereza itawapa mafunzo wanajeshi wa Ukraine kuhusu jinsi ya kutumia ndege za kivita za kawaida za Jumuiya ya kujihami ya NATO.

Baadaye, Zelensky amekutana na Mfalme Charles III wa Uingereza katika makao ya kifalme Birmingham London

Akikamilisha ziara yake mjini London, Rais Zelensky anatarajiwa kuwasili Paris Ufaransa baadaye leo. Ikulu ya rais wa Ufaransa imesema.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya, wanatumai, hapo kesho Zelensky atakuwa mgeni wao katika bunge lao mjini Brussels kukutana na viongozi wa umoja huo, katika kile ambacho zaidi itakuwa tukio la ishara, lakini ziara ambayo imetarajiwa baada ya miezi kadhaa ya muungano huo kuiunga mkono Ukraine.

(Vyanzo: APE,AFPE)