1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Kyiv

3 Februari 2023

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watakutana na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwa mkutano wa kilele mjini Kyiv wakiwa na ahadi ya vikwazo vipya dhidi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4N39E
Von der Leyen mit EU-Kommission zu Gesprächen in Kiew
Picha: Ukraine Presidency/dpa/picture alliance

Duru za habari zikiwanukuu maafisa wa Umoja wa Ulaya zinasema mkutano huo wa leo kati ya rais Zelensky na Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya utagusia masuala muhimu ikiwemo nyongeza ya msaada wa silaha na fedha kwa Ukraine pamoja na kurahisisha bidhaa za Ukraine kulifikia kwa urahisi soko la Umoja wa Ulaya.

Viongozi hao pia watazungumzia njia za kufidia mahitaji ya sasa ya nishati nchini Ukraine inayopatikana kwa shida tangu hujuma za vikosi vya Urusi kuisambaratisha miundombinu ya umeme ya nchi hiyo.

Kutakuwa pia na mjadala juu ya vikwazo ziada dhidi ya Urusi na utaratibu wa kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola watawala mjini Moscow wanaoshukiwa kwa uhalifu wa kivita.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen yuko mjini Kyiv tangu jana alikowasili kwa treni, katika safari iliyonuiwa kuwa ishara ya kuonesha uungaji mkono kwa taifa hilo linaloelekea kuadhimisha mwaka mmoja tangu uvamizi wa Urusi.

Bibi von der Leyen atajiunga na rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel kwa mkutano wa leo na rais Zelenksy utakaofanyika baada ya mazungumzo ya maafisa waandamizi kutoka pande zote mbili.

Bado hakuna ahadi kwa Ukraine kujiunga Umoja wa Ulaya 

Ingawa ishara zote zinaonesha kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi, taarifa zimedokeza kwamba awamu hiyo mpya haitokidhi mapendekezo yote yaliyotolewa na serikali ya rais Zelenky.

Von der Leyen mit EU-Kommission zu Gesprächen in Kiew
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, yuko mjini Kyiv na siku ya Alhamisi alikutana na rais Volodomyr Zelensky.Picha: Uncredited/Ukrainian Presidential Press Office/AP/dpa/picture alliance

Hata hivyo ahadi ya Ukraine kujiunga haraka ndani ya Umoja wa Ulaya, siyo miongoni mwa ahadi zitakazotolewa na viongozi wa Umoja huo watakapokutana na Zelensky mjini Kyiv.

Suala hilo ni miongoni mwa shauku kubwa alizonazo rais Zelenksy lakini watawala mjini Brussels wametanabahisha tangu mwanzo, kuwa mchakato wa nchi hiyo kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya utachukua muda mrefu.

Rais Putin atishia kujibu vikali dhidi ya taifa litakaloitisha Urusi 

Mkutano huo wa mjini Kyiv unafanyika siku moja baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kuapa kuwa atajibu vikali dhidi ya taifa lolote linalotishia usalama wa Urusi.

Russland | Putin zum 80. Jahrestag am Stalingrad Denkmal
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiweka shada la maua kuadhimisha miaka 80 ya mapambano ya kuwania mji wa Stalingrad wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.Picha: DMITRY LOBAKIN/AFP

Rais Putin alikuwa akizungumza kwenye kumbukumbu ya miaka 80 tangu jeshi la uliokuwa Muungano wa Kisovieti kupata ushindi dhidi ya vikosi vya Ujerumani kwenye mapigano ya kuwania mji Stalingrad mashariki mwa Urusi.

Alitumia hotuba hiyo pia kuikosoa Ujerumani kwa uamuzi wake wa kuipatia Ukraine vifaru vya kisasa vya Leopard 2. Ameifananisha hatua hiyo kuwa sawa na kitisho kipya kutoka kwa Ujerumani kama ilivyokuwa wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.

Hotuba hiyo ya Putin ilifuatia tahadhari iliyotolewa na rais Zelensky aliyesema kwamba Moscow inaimarisha nguvu ya vikosi vyake ili kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi nchini Ukraine.