1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa amefariki dunia

24 Julai 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametangaza siku 7 za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha rais mstaafu wa awamu ya tatu ya taifa hilo, Benjamin William Mkapa.

https://p.dw.com/p/3fqTB
Der frühere Präsident Tansanias Benjamin Mkapa
Picha: Abbas Mbazumutima/Iwacu

Mkapa aliyekuwa na umri wa miaka 81, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo wakati akipatiwa matibabu jijini Dar es Salaam. Huu ni msiba mwingine mkubwa wa kitaifa baada ya ule wa aliyekuwa rais wa kwanza wa taifa hilo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambao ulitokea Oktoba 14, 1999. Katika kipindi chote hiki cha maombelozo nchini Tanzania bendera zitapepea nusu mlingoti huku baadhi ya vyombo vya habari vikiwemo vya serikali pamoja na vile vya binafsi vikisikika kupiga nyimbo za maombolezo.

Usiku wa majonzi kwa Watanzania

Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John MagufuliPicha: DW/E. Boniphace

Saa 6 dakika 25 usiku wa kuamkia leo,(24.07.2020)  akionekana mwenye majonzi makubwa Rais Magufuli alisikika kupitia kituo cha televisheni kinachomilikiwa na chama tawala cha Channel 10 akisema " Mkapa amefariki dunia hospitalini jijini Dar es Salaam"

Aidha Rais Magufuli amewaomba Watanzania wote kuendelea kuwa watulivu na wamoja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi cha kuondokewa na mpendwa wao, Rais Mstaafu Mkapa.

Mkapa ambae alizaliwa 1938 mjini Ndanda, karibu na Masasi huko kusini mwa Tanzania na alihudumu nafasi ya urais wa taifa hilo katika kipindi cha 1995  hadi 2005, nyadhfa ambayo ilikwenda  karibu na muda unaokaribiana na nafasi yake ya uenyekiti wa chama tawala cha taifa hilo CCM. Alihitimu shahada yake ya mwanzo katika Chuo Kikuu Cha Makerere cha nchini Uganda na baadae Chuo Kikuu cha Columbia, ambapo alipata shahada ya uzamili katika taalumu ya mahusiano ya umma.

Soma zaidi:Mazungumzo ya kutafuta amani Burundi yaanza Arusha

Katika wakati wa uhai wake amewahi kupata nyadhfa mbalimbali katika ngazi ya mikoa na serikali ya Tanzania zikiwemo wizara ya Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu, Wizara ya Mambo ya Nje. Na katika zama za utawala wake kama rais, pamoja na masuala mengine ya jitihada za upatanishi atakumbukwa na hatua za ubinafshaji wa mashirika ya umma nchini Tanzania ambayo ilipokewa kwa mawazo tofauti

Vyanzo: Reuters, Ikulu ya Tanzania