Mazungumzo ya kutafuta amani Burundi yaanza Arusha | Matukio ya Afrika | DW | 25.10.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mazungumzo ya kutafuta amani Burundi yaanza Arusha

Mazungumzo ya amani kwa Burundi yameanza tena mjini Arusha, lakini bila ya ushiriki wa serikali.

Mazungumzo ya awamu ya tano na ya mwisho ya kutafuta amani nchini Burundi yameanza leo jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania bila ushiriki wa serikali ya taifa hilo na kushuhudia msuluhishi msaidizi wa mgogoro huo rais mstaafu wa Tanzania Benjamen Mkapa anayeongoza mazungumzo hayo akitupa lawama za wazi kwa serikali hiyo kukwaza juhudi za kuleta maridhiano miongoni mwa raia wa taifa hilo. 

Katika hotuba yake fupi ya ufunguzi wa mazungumzo hayo mapema leo msuluhishi huyo ambaye pia ni rais mstaafu wa Tanzania amesema kuwa amefanya jitihada zote zilizo ndani ya uwezo wake kuhakikisha kuwa serikali ya Burundi inashiriki katika mazungumzo hayo lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda hatua ambayo imekwaza maendeleo ya mazunguzo hayo.

Msuluhishi huyo aliongeza kuwa serikali ya Burundi mara kwa mara imekuwa ikitoa masharti na kutaka mazungumzo hayo kuahirishwa.

Mkapa atoa wito kwa washiriki kuwa huru kutoa mapendekezo

Mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Burundi ulianza mwaka 2015 kufuatia uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu

Mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Burundi ulianza mwaka 2015 kufuatia uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu

Hata hivyo Mkapa amesema mazungumzo hayo yataendelea na amewataka washiriki kuwa huru kujadili na kutoa mapendekezo wanayo amini kuwa yataweza kuleta amani ya kudumu katika taifa la Burundi na kuhakikisha kuwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2020 unakuwa huru na wa haki.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na wawakilishi wa makundi ya kijamii ,vyombo vya habari,mashirika ya kiraia ,wanasiasa wa ndani na waishio uhamishoni na wawakilishi wa viongozi wa dini kutoka nchini Burundi na kushuhudiwa waangalizi wa kikanda na kimataifa.

Mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Burundi ulianza mwaka 2015 kufuatia uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu na kupelekea kutokea machafuko yaliyogaharimu maisha ya mamia ya watu huku wengi wakikimbilia uhamishoni.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga