1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin njiani kushinda muhula wa nne madarakani

18 Machi 2018

Raia wa Urusi wanapiga kura Jumapili hii katika uchaguzi wa rais ambamo rais wa sasa Vladmir Putin anao uhakika wa kushinda muhula wa nne. Putin aliekuwa madarakani kwa karibu miongo miwili, alipiga kura mjini Moscow.

https://p.dw.com/p/2uXdp
Russland Wahlen
Picha: picture-alliance/Mikhail Metzel/TASS/dpa

"Nina uhakika kuwa mpango nilioupendekeza kwa nchi ni sahihi," Putin alinukuliwa akisema na shirika la habari la Interfax.

Uchaguzi huo unafanyika mnamo wakati mgogoro unafukuta kati ya Urusi kwa upande mmoja, na Uingereza na washirika wake kwa upande mwingine kuhusiana na matumizi ya sumu iliyotengenezwa nchini Urusi dhidi ya jasusi wa zamani na Uingereza na binti yake katika mji wa Uingereza wa Salisbury. Urusi imekanusha ushiriki wowote katika tukio hilo.

Uchaguzi huo pia unafanyika katika siku ya kumbukumbu ya mwaka wa nne tangu Urusi ilipoitwa rasi ya Crimea kutoka Ukraine, hatua ambayo ilichukuliwa na Urusi kama kichocheo kwa umaarufu wa Putin ambao tayari ulikuwa imara.

Ameendelea kuwa na umaarufu wa asilimia 70 katika miaka ya karibuni, kwa mujibu wa tafiti za maoni ya raia zilizofanyika nchini kote na mashirika mawili makubwa zaidi ya utafiti nchini humo, moja la kiserikali na lingine la binafsi.

Muda wa utawala wa Putin hata hivyo, umezusha uvumi kwamba wapigakura wengi huenda wakajizuwia kushiriki uchaguzi huu ambao matokeo yake yanaonekana kutabirika kwa kiasi kikubwa. Chini ya katiba kama ilivyo sasa, muhula wa nne ndiyo wa mwisho kwake.

Russland Wahlen
Orodha ya wagombea urais kama ilivyoonekana wakati wa zoaezi la kupiga kura katika kituo cha kupigia kura. Kibao cha nyuma kinasomeka "Kwa ajili ya Urusi."Picha: picture-alliance Donat Sorokin/TASS/dpa

Uchaguzi huo ulipangwa kumalizika wakati vituo vya kupigia kura vitakapofungwa katika mkoa wa Kalinigrad ulioko mbali magharibi mwa Urusi majira ya mbili za usiku. Urusi ndiyo nchi kubwa zaidi duniani na inazo zoni 11 za wakati. Karibu wapigakura milioni 109 wana vigezo vya kupiga kura.

Mmoja wa wakosoaji wakubwa zaidi wa Putin, kiongozi wa maandamano Alexei Navalny, alizuwiwa kugombea katika uchaguzi huo kutokana na kutiwa hatiani kwa makosa ya kifedha, ambayo anayapinga kwa madai kuwa yalipangwa tu. Navalny aliwatolea mwito Warusi kususia uchaguzi huo na kueleza matumani kuwa utadhoofishwa na uitikiaji mdogo.

Wapinzani wakuu watatu wa Putin, kwa mujibu wa kura za maoni, walikuwa Pavel Grudini wa chama cha Kikomunisti, Mzalendo Vladmir Zhironovsky, na mwanahabri aliegeuka msoshalisti Ksenia Sobchak. Lakini wako nyuma kabisaa ya Putin wakiwa na umaarufu wa tarakimu moja tu katika utafiti wa maoni ya wapigakura.

Jaribio la udukuzi wa tovuti ya uchaguzi

Tume ya uchaguzi ya Urusi imesema tovuti yake ililengwa katika jaribio lililofeli la udukuzi wakati wa zoezi la upigaji kura la Jumapili. Mwenyekiti wa tume hiyo Ella Pamfilova aliwaambia waandishi habari kwamba jaribio hilo lilifuatliwa na kuhusishwa na kompyuta katika mataifa 15, bila kuyataja mataifa hayo. Mashambulizi kama hayo ni ya kawaida.

Alisema juhudi za kuvuruga tovuti hiyo zilitokea wakati wapigakura katika eneo la mbali la mashariki mwa Urusi wameanza kupiga kura, lakini zilizuwiwa na maafisa wa Urusi.

Wakati Marekani ikichunguza madai ya udukuzi wa Urusi na uingiliaji mwingine katika ushindi wa rais Donald Trump katika uchaguzi wa 2016, maafisa wa Urusi wamedai pia kwamba mataifa ya kigeni yanajaribu kuingilia uchaguzi wa Jumapili.

Bild Zeitung Wahlen in Russland BILD gratuliert Putin zu seinem Sieg vor der Wahl
Gazeti la Bild la Ujerumani limempongeza Vladmir Putin kwa ushindi hata kabla ya uchaguzi kukamilika.Picha: DW

Warusi wazuwiwa kupiga kura Ukraine

Vikosi vya usalama viliyazingira majengo ya Urusi nchini Ukraine huku kukiwa na hasira juu ya hatua ya serikali ya Ukraine kukataa kuwaruhusu Warusi wa kawaida kumchagua rais.

Vikosi vya polisi viliripotiwa kuulinda ubalozi wa Urusi mjini Kiev pamoja na ofisi za ubalozi mdogo katika mji wa Odessa na miji mingine. Serikali ya Ukraine ilitangaza kuwa ni maafisa wa diplomasia wa Urusi tu watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi wa Jumapili. Mamilioni ya watu wenye asili ya Urusi wanaishi nchini Ukraine lakini idadi ya wapigakura wa Urusi walioandikishwa nchini Ukraine haijulikani.

Ukraine inapinga upigaji kura katika rasi ya Crimea, iliyotwaliwa kimabavu na Urusi miaka minne iliyopita. Ukraine pia inaghadhabishwa na uungaji mkono wa Urusi kwa waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine, ambako mgogoro wa umwagaji damu unaendelea.

Kwa mujibu wa mashirika ya habari ya Urusi, maafisa wa serikali ya Urusi wameuomba Umoja wa Mataifa na Baraza la Ulaya kuigilia kati.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DPAE, APE

Mhariri: Sylvia Mwehozi