1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin aionya Magharibi kuhusu kitisho cha vita vya nyuklia

29 Februari 2024

Rais wa Urusi Vladmir Putin ameonya leo kuhusu hatari halisi ya kuzuka vita vya nyuklia kama nchi za Magharibi zitaendelea kujiingiza katika vita vya nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4d2W7
Urusi Volgograd | Hotuba ya Rais Vladimir Putin kwa njia ya Vidio
Rais Putin amesema hata wao wanazo silaha nzito wanazojivunia nazo Magharibi.Picha: Dmitry Rogulin/TASS/dpa/picture alliance

 Akizungumza mjini Moscow katika hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa, Putin amesema wanajeshi wake wanaendelea kusonga mbele nchini Ukraine na kuzionya nchi za Magharibi kuhusu madhara makubwa kwa nchi yoyote itakayothubutu kuwapeleka askari nchini Ukraine.

"Nasi pia tunazo silaha, - wanajua kuhusu hili, kama nilivyosema hivi punde, - pia tuna silaha ambayo inaweza kuyapiga maeneo yao. Na (wanapaswa kuelewa) kwamba wanachokifanya sasa kujaribu kuutisha ulimwengu wote – kinaweza kuzusha mzozo wa silaha za nyuklia. Kumaanisha maangamizo ya ulimwengu. Je, hawaelewi hili, au nini?"

Urusi | Putin atoa hotuba ya taifa
Rais Putin pia amesifu maendeleo ya vikosi vyake katika uwanja wa vita nchini Ukraine.Picha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Kauli zake zimeonekana kuwa jibu kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye mapema wiki hii alikataa kufuta uwezekano wa kuwapeleka wanajeshi nchini Ukraine -- mtizamo ambao ulizusha upinzani wa haraka kutoka kwa viongozi wengine wa Ulaya.

Putin pia alipongeza hali nzuri ya kiuchumi ya Urusi na kuelezea mageuzi kadhaa madogo madogo ya ndani kama sehemu ya ahadi zake kwa Warusi kabla ya uchaguzi wa rais wa mwezi ujao ambao anatarajiwa kupata ushindi rahisi.