1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wawili wajeruhiwa katika maandamano Marekani

Josephat Charo
24 Septemba 2020

Maafisa wawili wa polisi wamepigwa risasi na kujeruhiwa Jumatano jioni mjini Louisville jimbo la Kentucky nchini Marekani wakati wa maandamano kufuatia uamuzi wa mahakama kuhusu kisa cha Breonna Taylor

https://p.dw.com/p/3iwKn
USA | Kentucky | Fall Breonna Taylor | Protest
Picha: Bryan Woolston/Reuters

Maafisa wawili wa polisi wamepigwa risasi na kujeruhiwa Jumatano jioni mjini Louisville jimbo la Kentucky nchini Marekani wakati wa maandamano kufuatia uamuzi wa mahakama uliokosolewa na wanaharakati wa haki za kiraia kama kosa kubwa la ukiukaji na unyimaji wa haki katika tukio la kupigwa risasi na kuuwawa Breonna Taylor mnamo mwezi Machi mwaka huu. Soma pia: Trump: Maandamano ya mjini Kenosha ni 'ugaidi wa ndani'

Mahakama iliamua kwamba kati ya maafisa watatu waliohusika na uvamizi wa polisi katika makazi ya Taylor, hakuna hata mmoja atakayeshtakiwa kwa kusababisha kifo cha mwanamke huyo, ingawa afisa mmoja alitiwa hatiani kwa kuhatarisha maisha ya majirani wa Taylor.

USA BlackLivesMatter | Protest gegen den Tod von Breonna Taylor in Louisville
Maandamanoya kupinga ukatili wa polisi MarekaniPicha: Reuters/B. Woolston

Uamuzi huo umetolewa zaidi ya miezi sita tangu Taylor, fundi mtaalamu wa vifaa vya matibabu aliyekuwa na ndoto ya kuwa muuguzi na aliyekuwa na umri wa miaka 26, alipouliwa mbele ya mpenzi wake aliyekuwa amejihami na silaha, wakati maafisa watatu walipoingia nyumbani kwake kwa kutumia nguvu wakiwa na waranti wa kufanya msako kuhusiana na uchunguzi wa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Kufuatia tangazo la mahakama, waandamanaji mara moja walijitokeza kwa wingi katika barabara za mji mkubwa wa jimbo la Kentucky, Loiusville, na kuandamana kwa saa kadhaa wakipiga kelele wakisema: "Hakuna maisha yenye thamani mpaka maisha ya watu weusi yatakapokuwa na thamani". Kulishuhudiwa matukio ya baadhi ya waandamanaji kupigana vikumbo na maafisa wa polisi, huku maandamano hayo yakifanyika kwa kiwango kikubwa kwa njia ya amani, hadi pale risasi zilipoanza kurindima wakati maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami na silaha nzito walipowakabili waandamanaji na kuwataka wavunje maandamano yao mida ya saa mbili na nusu usiku kabla ya saa za msako kuanza saa tatu kamili. Soma pia:Trump asaini sheria ya polisi baada ya shinikizo la waandamanaji

Mwandishi wa shirika la habari la Reuters aliyekuwa katika eneo la tukio anasema alisikia mlio wa risasi kutoka upande wa waandamanaji muda mfupi baada ya polisi kuwarushia gesi za kutoa machozi. Kaimu msemaji wa jeshi la polisi wa mji wa Louisville, Robert Schroeder, amethibitisha maafisa wawili wamepigwa risasi, lakini hawako katika hali taabani ya kutia wasiwasi kuhusu maisha yao.

"Mwendo wa saa mbili na nusu usiku maafisa wetu waliitwa kwenda eneo la Brook na East College kulikokuwa na kundi kubwa la watu na risasi zikifyetuliwa. Walipofika na kuanza kuchunguza kilichokuwa kikiendelea risasi zilifyetuliwa na maafisa wetu wawili wakapigwa risasi. Wote wanatibiwa katika hospitali ya chuo kikuu. Mmoja hali yake ni nzuri na mwingine anafanyiwa upasuaji, lakini pia yuko katika hali nzuri."

USA Breonna Taylor-Fall in Louisville
Tamika Palmer, mamake Breonna TaylorPicha: Reuters/B. Woolston

Schroeder aidha amesema mshukiwa mmoja ametiwa mbaroni. Mgombea urais wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa Novemba 3, Joe Biden, amewatolea wito watu wanaoandamana kupinga uamuzi wa mahakama kuhusu Breonna Taylor wasifanye fujo. Akizungumza jana mjini Charlotte katika jimbo la North Carolina, Biden alisema: "Jambo ninalotaka kuliweka bayana ni kwamba kuandamana kunaingia akili. Ni wazi watu wanatakiwa kuwa na uhuru wa kuzungumza, lakini bila kufanya machafuko. Hakuna kufanya machafuko. Pole zangu zimwendee mama yake Breona Taylor. Kitu cha mwisho anachotaka kukiona ni machafuko barabarani. Kwa hiyo andamaneni kwa amani. Msifanye machafuko."

Mapema jana watu kadhaa waliswekwa ndani na polisi kufuatia makabiliano kati ya mamia ya waandamanaji na kundi la maafisa wa usalama katika kitongoji cha Highlands nje ya mji wa Lousville. Baadhi ya madirisha ya majumba ya biashara yaliyo karibu pia yalivunjiliwa mbali. Polisi wanasema watu wapatao 46 walikamatwa.

reuters, aptn,