1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asaini sheria ya polisi baada ya shinikizo

Mohammed Khelef
17 Juni 2020

Kufuatia maandamano ndani na nje ya Marekani kupinga ubaguzi na ukatili wa polisi dhidi ya watu weusi, hatimaye Rais Donald Trump amesaini sheria ambayo anasema itawashajiisha polisi kutenda vyema zaidi kazi zao.

https://p.dw.com/p/3duX6
USA Trump unterschreibt Ausführungsverordnung zur sicheren Polizeiarbeit
Picha: picture-alliance/CNP/MediaPun/S. Reynolds

Trump alikutana na familia za baadhi ya Wamarekani weusi waliouawa na polisi kabla ya sherehe za kusaini sheria hiyo, akisema kwamba anahuzunishwa na maisha yaliyopotea na familia zilizosambaratishwa kwa mauaji hayo. Lakini punde akabadilisha mahadhi ya sauti yake, akijielekeza kwenye umuhimu wa raia kuwaheshimu walinda usalama na kufuata sheria:

"Wamarekani wanataka utawala wa sheria. Wanahitaji utawala sheria. Wanaweza wakawa hawasemi hilo, wanaweza wakawa hawazungumzii hilo, lakini hilo ndilo walitakalo. Wengine hata hawajuwi walitakalo, lakini ni hilo ndilo walitakalo. Na wanalifahamu hilo pale unapowaondosha polisi, maana unawaumiza zaidi wale wasiokuwa na kitu;" alisema.

Trump aliwaelezea maafisa wa polisi waliotumia nguvu za ziada kuwa ni wachache sana kati ya wale wengi ambao ni waaminifu kwa sheria na haki za raia.

Akiwa amezungukwa na maafisa wa polisi katika tafrija hiyo ya Rose Garden, kiongozi huyo anayewania kusalia madarakani kwa muhula wa pili na wa mwisho alisema kupunguza uhalifu na kuinuwa hali ya maisha ya watu si malengo yanayokinzana, hapana shaka akielekeza kauli yake kwa jamii kubwa ya Wamarekani weusi ambao kiwango cha uhalifu na umasikini vinalingana. 

Familia hazijatosheka

USA Washington | Polizeidekret | Donald Trump
Rais Trump akionesha sheria mpya aliyoisaini.Picha: picture-alliance/dpa/S. Reynolds

Hata hivyo, wakili wa familia za Wamarekani Weusi waliouawa mikononi mwa polisi, S. Lee Merritt, alisema hotuba ya Trump pamoja na sheria aliyoisaini havijatatuwa suala la msingi linalopelekea wahanga wa ubaguzi wa rangi kuendelea kuwa wahanga nchini Marekani.

"Amebainisha sheria yake ambayo lazima niseme kwamba ni tupu. Hamuna chochote ndani yake ambacho familia hizi zitasema kingeliweza kuhakikisha kuwa Atatiana Jefferson asingeuliwa nyumbani kwake au kwamba Botham Jean angeweza kuishi au kwamba kungelikuwa na hukumu kubwa zaidi kwa Amber Guyger kwa mauaji yake. Hamuna chochote kwenye sheria hii ambacho tunaweza kuondoka nacho hapa na kuhisi kwamba kimelipa maana vuguvugu letu." Alisema mwanasheria huyo.

Trump na wajumbe wa chama chake cha Republican katika Baraza la Congress wamekuwa wakiharakisha kuchukuwa hatua za kukabiliana na ghadhabu za umma dhidi ya ukatili wa polisi na dharau zenye misingi ya ubaguzi wa rangi, kufuatia kifo cha George Floyd, Mmarekani mweusi aliyefia mikononi mwa polisi pamoja na Wamarekani wengine wa jamii yake. 

Wengi wanasema sheria hii mabadiliko ya ghafla katika kundi la wanasiasa wahafidhina, ambayo yanaashiria ni kwa namna gani maandamano yanaweza kubadili mwenendo wa siasa na kuilazimisha Ikulu ya White House na Baraza la Congress kuchukua hatua za haraka.