1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Maandamano ya mjini Kenosha ni 'ugaidi wa ndani'

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
2 Septemba 2020

Licha ya kuambiwa asiende kwenye mji wa Kenosha, rais Trump aliwasili katika mji huo siku ya Jumanne. Katika upande mmoja alipokelewa kwa maandamano ya kumpinga na pia walikuwapo waliomuunga mkono.

https://p.dw.com/p/3htk8
USA Präsident Trump in Kenosha
Picha: Reuters/L. Mills

Rais Donald Trump Jumanne alipeleka ujumbe wake makhsusi wa kusisitiza kuzingatia sheria katika jiji la Kenosha, ambapo aliyaelezea maandamano ya hivi karibuni ya kupinga ubaguzi wa rangi kuwa ni vitendo vya ugaidi wa ndani ya nchi vinavyofanywa na makundi ya watu wanaopendelea kuzusha vurugu.

Rais Trump anasema kusudio la safari yake hiyo lilikuwa kujionea yaliyotokea na pia kuwashukuru polisi kwa kuilinda jamii. Alisema ili kumaliza vurugu lazima tukabiliane na matendo yote yanayohusiana na  itikadi kali, na hapo hapo akawalaumu wanasiasa wanaotoa ujumbe unaosababisha madhara. Katika mkutano huo Mwanasheria Mkuu William Barr, kaimu Katibu wa Idara ya Usalama wa Taifa Chad Wolf, na wachungaji wa kanisa analohudhuria  mama yake Jacob Blake walikuwepo kwenye ukumbi huo.

Wamarekani wadai haki itendeke kutokana na kifo cha Jacob Blake
Wamarekani wadai haki itendeke kutokana na kifo cha Jacob BlakePicha: Getty Images/M. M. Santiago

Rais Trump binafsi hakuzungumza na familia ya Blake lakini alisema anasikitishwa sana na matukio kama hayo kwa mtu yeyote yule. Alimpongeza mkuu wa polisi wa jiji la Kenosha David Beth, ambaye anakosolewa kwa kauli aliyotoa juu ya kuwahifadhi watu wanaoshukiwa kuhusika katika uhalifu ili wasiweze kuzaa tena.

Wanachama wa chama cha Democratic na watetezi wanaotaka mageuzi kwenye idara ya polisi wanauona mji wa Kenosha kama ishara ya taasisi ya ubaguzi wa rangi. Trump, hata hivyo ana kipaumbele tofauti, anapinga kile ambacho amekielezea mara kwa mara kama machafuko katika miji inayoongozwa na Wademocrat. Amesema Wamarekani wanapaswa kulaani kauli kali dhidi ya polisi.

Gavana wa jimbo la Wisconsin na meya wa Kenosha, wote wa chama cha Democratic, walimsihi Trump asiutembelee mji huo lakini alipuuza ombi lao. Joe Biden amemlaumu rais Trump kwa kuchochea ghasia kwa makusudi ili kujinufaisha kisiasa. Vurugu za wiki iliyopita huko Kenosha zilikumbushia maandamano ya miezi kadhaa ya kuwapinga polisi na ubaguzi wa rangi, yaliyosababishwa na kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd ambaye hakuwa na silaha. Alikufa mikononi mwa polisi katika mji wa Minneapolis.

Vyanzo: AFP/DW