Obama azindua mpango wa kudhibiti bunduki | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama azindua mpango wa kudhibiti bunduki

Rais Barack Obama wa Marekani amelitaka bunge la nchi hiyo kupitisha sheria inayopiga marufuku uuzaji wa bunduki zilizoundwa kwa matumizi ya kivita, na utaratibu wa kukagua historia ya kila mtu anayetaka kununua bunduki.

Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani

Hatua hiyo ya Obama iko katika juhudi za kudhibiti umilikaji holela wa bunduki baada ya visa vingi vya mauaji ya kutumia silaha hiyo, hususan mauaji yaliyofanywa kwenye shule katika mji wa Newtown hivi karibuni.

''Kama kuna kitu ambacho twaweza kukifanya kupunguza kiwango hiki cha fujo, hata kama ni kimoja, kama tunaweza kuokoa maisha hata ya mtu mmoja, tunalo jukumu la kujaribu, na nitatekeleza jukumu langu''. Alisema rais Barack Obama mbele ya mkutano wa waandishi wa habari mjini Washington, akitangaza mpango huo.

Obama alilitaka bunge kutoukwamisha mpango wake, na kupuuza kilio cha wananchi. Mpango huo unatabiriwa kuanzisha mapambano na makundi yanayounga mkono uhuru wa kumiliki silaha, ambayo yana nguvu katika siasa za Marekani.

Mamlaka ya urais yatumika

Rais Obama alisaini maagizo 23 akitumia mamlaka ya rais, katika juhudi za kudhibiti mauaji yanayofanywa na watu wenye bunduki baada ya mauaji ya watoto 20 na watu wazima sita kwenye shule ya Sandy Hook katika mji wa Newtown jimboni Connecticut mwezi uliopita.

Wahafidhina nchini Marekani huuchukulia umiliki wa bunduki kama haki yao ya msingi

Wahafidhina nchini Marekani huuchukulia umiliki wa bunduki kama haki yao ya msingi

Alilitaka bunge kukubali mapendekezo ya kupiga marufuku uuzaji wa silaha zilizotengenezwa kwa matumizi ya kijeshi, ku kuziba pengo katika katika sheria ambalo linawezesha asilimia 40 ya bunduki zinazouzwa kuangukia mikononi mwa watu ambao historia ya mienendo yao haijulikani.

Msuguano na wahafidhina

Obama alikiri katika hotuba yake kwamba kuna changamoto kubwa katika kufanikisha mpango wake huo, na kuongeza kuwa mpira sasa uko katika uwanja wa bunge.

''Mageuzi makubwa tunayoweza kuyafanya yatategemea uamuzi wa bunge. Wabunge wanapaswa kuupigia kura mpango huu, na wananchi hawana budi kuhakikisha kuwa hilo linafanyika. Naomba nieleweke, waulize wawakilishi wenu kama wamepiga kura kuondoa bunduki mikononi mwa watu wabaya.'' Alisema rais Obama.

Chama cha wamiliki wa bunduki, NRA, kinatarajiwa kuwa kikwazo kikubwa kwa mpango wa Obama

Chama cha wamiliki wa bunduki, NRA, kinatarajiwa kuwa kikwazo kikubwa kwa mpango wa Obama

Upande unaonyoshewa kidole kuwa kizingiti kikubwa katika kufanikiwa kwa mpango huo kuhusu udhibiti wa silaha, ni makundi ya wakereketwa wa uhuru wa kumiliki bunduki, hasa chama cha kitaifa cha wamiliki wa bunduki, NRA. Obama alisema alitegemea kuwa watu hao watafanya kila njia kuuonyesha mpango huo kuwa wa waliberali wanaotaka kukandamiza uhuru wa wamarekani.

Tayari mpango huo wa rais Obama umekwishakosolewa na wahafidhina katika chama cha Republican, ambao wamesema unalenga haki ya kumiliki silaha. Kiongozi wa Seneti ya Marekani Harry Reid ambaye ni kutoka chama cha Democratic cha rais Obama ameukaribisha mpango huo aliouta wenye kufikiriwa kwa makini, lakini hakutangaza chochote atakachokifanya.

Ingawa sheria ya kuchunguza mienendo ya wanunuzi wa silaha inaweza kuungwa mkono, sheria ya kupiga marufuku bunduki zenye uwezo wa kijeshi inaweza kupingwa hata na wabunge wa chama cha Democratic wanaotoka katika majimbo ya wahafidhina, kwa hofu ya kuwakasirisha wapiga kura katika uchaguzi wa katikati mwa muhula ambao utafanyika mwaka 2014.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri:Idd Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com