Netanyahu akubali kujiunga na Bodi ya Amani ya Gaza
21 Januari 2026
Hivi karibuni Israel ilionesha kutokuridhshwa na hatua ya Marekani kuchukua jukumu kubwa katika chombo cha kimataifa cha kusimamia Ukanda wa Gaza. Netanyahu anatajwa kukasirishwa na uwepo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan na mwakilishi wa ngazi ya juu wa Qatar Ali al-Thawadi katika bodi hiyo. Itakumbukwa kuwa Uturuki na Qatar zilikosoa vikali vita vya Israel dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo, vikosi vya Israel vimeziamuru makumi ya familia za Kipalestina zinazoishi kusini mwa Gaza kuondoka kwenye makazi yao. Kulingana na wakaazi wa eneo la Bani Suhaila, mashariki mwa Khan Younis, jeshi la Israel lilidondosha vipeperushi katika kitongoji cha Al- Reqeb na kuwataka watu waondoke mara moja.
Israel yakanusha kutaka kuwaondoa kwa nguvu makwao Wapalestina
Jeshi la Israeli limesema halina mpango wa kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina kutoka eneo hilo lakini limekiri kuwa vipeperushi vyake vililenga kuwaonya Wapalestina wasivuke mpaka wa eneo la vita uliowekwa. Hii ni mara ya kwanza kwa Wapalestina kuhamishwa kwa nguvu tangu makubaliano ya kusitisha vita yalipoanza kutekelezwa mwezi Oktoba mwaka uliopita.
Huku hayo yakiendelea, polisi nchini Israel wameingia kwa nguvu katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA na kuanza kuyabomoa majengo yake mashariki mwa Jerusalem.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia naibu msemaji wake, Farhan Haq ameonya akisema kuwa, ofisi za UNRWA ni ofisi za Umoja wa Mataifa hivyo, shambulio dhidi ya UNRWA ni shambulio dhidi ya Umoja wa Mataifa. Amesema mashambulizi hayo hayapaswi kukaliwa kimya.
Haq ameongeza kusema kuwa Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa Israel kusitisha mara moja shughuli hiyo ya kuyabomoa majengo ya shirika hilo ambalo Israel imekuwa ikilishutumu kwa kuwahifadhi wanachama wa kundi la Hamas.