Nchi za Ziwa Tanganyika zatakiwa kushirikiana | Matukio ya Afrika | DW | 13.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Nchi za Ziwa Tanganyika zatakiwa kushirikiana

Serikali ya Burundi imeitolea wito Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kujiunga na nchi za afrika mashariki ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, uchumi na usalama katika eneo la ziwa Tanganyika.

Rai hiyo ilitolewa na Balozi mdogo wa Burundi nchini Tanzania Jean Bosco Ndayikengurukiye katika mahojiano maalumu na DW mkoani wa Kigoma.

Bwana Ndayikengurukiye alisema kuwa wakati nchi za Rwanda, Uganda na Kenya zikiishirikisha Sudani Kusini kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi nje ya mfumo wa ushirikiano wa Afrika mashariki, ipo haja kwa Tanzania, Burundi na DRC kuungana kiuchumi.

Kwa upande wake Balozi msaidizi wa ubalozi mdogo wa DRC nchini Tanzania Rickie Molema alikiri kuwepo kwa mipango ya nchi yake kujiunga na nchi za afrika mashairiki kiuchumi. Molema alisema kuwa serikali ya rais Joseph Kabila imeshafanya makubaliano kadhaa na Tanzania kama sehemu ya kufikia azima hiyo.

Makubaliano hayo yanahusisha miongoni mwa mambo mengine, ni pamoja na mamlaka ya bandari Tanzania TPA kufungua ofisi ndogo mjnini Lubumbashii nchini DRC.

Serikali za Burundi na DRC ziliipongeza Tanzania kwa kujenga miundo mbinu ya kiuchumi katika ukanda wa ziwa Tanganyika kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi za Burundi, DRC na Zambia.

Balozi Molema wa DRC pamoja na Balozi Ndayikengurukiye wa Burundi kwa pamoja waliitaja miradi mikubwa ya ujenzi wa bandari mpya ndani ya ziwa Tanganyika eneo la Kagunga mkoani Kigoma na ujenzi wa masoko ya ujirani mwema kama njia muhimu ya kukuza uchumi wa maeneo hayo.

Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA ilithibitisha kuanza kwa ujenzi wa bandari eneo la Kagunga mpakani wa Tanzania na Burundi ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo.

Mwandishi: Prosper Kwigize
Mhariri: Josephat Charo