Nani mwenye haki na maji ya mto Nile? | Matukio ya Afrika | DW | 26.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Nani mwenye haki na maji ya mto Nile?

Hivi karibuni Ethiopia huenda ikaanza kujaza bwawa lake kubwa la dola bilioni 4 mwaka huu, ingawa Msiri ina hofu kwamba bwawa hilo linaweza kuathiri usambazaji wa maji inaoutegemea kwa kilimo, viwanda na maji ya kunywa.

Wakati Ethiopia ikiashiria kwamba huenda ikaanza kujaza bwawa lake kubwa la dola bilioni 4 mwaka huu, hifadhi ya rasilimali adimu ya maji ya mto Nile imejitokeza kuwa ajenda ya juu ya kisera ya rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi wakati akianza muhula wake wa pili.

Nchi hizo mbili zimekuwa katika majadiliano ya ubishani kwa miaka kadhaa na bado hazijafikia makubaliano ya kugawana maji ya mto Nile.  Misri ambayo inategemea mto Nile kwa kiasi kikubwa kwa kilimo, viwanda na maji ya kunywa, imekuwa ikitafuta hakikisho kwamba bwawa hilo halitakata mtiririko wa maji kwa wakazi wake wanaozidi kuongezeka.

Ethiopia, ambayo nidiyo chanzo cha mto wa Blue Nile unaoungana na White Nile mjini Khartoum na kutiririka nchini Msiri, imesema kwamba bwawa hilo halitaathiri usambazaji huo na inatumaini kwamba mradi huo utaibadilisha nchi hiyo kuwa kitovu cha nguvu katika ukanda ulio na uhaba wa umeme.

Makubaliano ya maji ya mto Nile ya 1929

Merowe Staudamm im Sudan Chinesischer Arbeiter (picture-alliance/dpa)

Bwawa la Merowe nchini Sudan likijengwa katika mto Nile

Makubaliano ya mwaka 1929 yalisainiwa kati ya Misri na Uingereza, ambayo kwa wakati huo iliziwakilisha nchi za Uganda, Kenya, Tanganyika hivi sasa Tanzania na Sudan. Mkataba huo uliipatia Cairo haki ya turufu ya kupinga miradi mikubwa inayoathiri sehemu yake ya maji.

Makubaliano ya 1959 baina ya Misri na Sudan

Makubaliano haya baina ya Misri na Sudan, kuongezea makubaliano ya awali, yaliipatia Misri haki ya ujazo wa bilioni 55.5 mita za maji ya Nile kwa mwaka na Sudan mita za ujazo bilioni 18.5 kwa mwaka. Makubaliano yote ya mwaka 1929 na 1959 yametengeneza chuki miongoni mwa mataifa mengine yanayotumia mto Nile na kutoa wito wa mabadiliko katika mkataba huo, yanayopingwa na Misri.

Mpango wa matumizi ya bonde la mto Nile

Mpango huu ulianzishwa mwaka 1999, uliyaleta mataifa tisa ya bonde la Nile ili kuuendeleza mto huo katika mazingira ya ushirikiano, kushirikiana faida za kiuchumi na kukuza amani ya kikanda na usalama. Mpango wa nchi tisa za bonde la Nile zilikuwa ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ethiopia, Kenya, Sudan, Rwanda, Tanzania na Uganda. Tangu wakati huo Sudan Kusini nayo imeongezwa katika mpango huo.

Makubaliano ya Entebbe

BdT WM Qualifikation Ägypten Algerien Fußball (AP)

Familia nyingi za Misri zinategemea shughuli za uvuvi katika mto Nile

Misri iliondoa uanachama wake katika mpango wa bonde la mto Nile mwaka 2010 baada ya nchi nyingine kusaini mkataba wa makubaliano wa CFA. Misri inadai makubaliano hayo yaligawa upya matumizi ya maji ya mto huo bila ya ridhaa yake.

Mkataba wa CFA unaojulikana kama makubaliano ya Entebbe, ulisainiwa na nchi sita kati ya 10 za mpango wa bonde la mto Nile. Nchi hizo ni Uganda, Ethiopia, Rwanda, Tanzania, Kenya na Burundi.

Misri inataka mbadala wa mkataba huo, ambao sasa unaruhusu nchi nyingine kuanzisha miradi katika mto huo bila ya ridhaa yake.

Mkataba wa ushirikiano wa 2015

Viongozi kutoka Misri, Ethiopia na Sudan walitia saini mkataba wa ushirikiano mwaka 2015 juu ya ujenzi wa bwawa kubwa katika jitihada kupunguza mvutano. Mkataba huo ulilenga kusafisha njia kwa ajili ya ushirikiano wa baadae wa kidiplomasia. Kanuni kuu katika makubaliano hayo ni pamoja na kutoa kipaumbele kwa nchi kutumia umeme utakaozalishwa katika bwawa hilo, njia inayoonekana kutatua migogoro na kutoa fidia kwa uharibifu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com