Mtuhumiwa mkuu wa kundi la kigaidi la NSU afungwa maisha | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.07.2018

Tembelea tovuti mpya ya DW

Tazama toleo la beta la dw.com. Bado hatujamaliza! Maoni yako yanaweza kutusaidia kuiboresha.

  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

MUNICH

Mtuhumiwa mkuu wa kundi la kigaidi la NSU afungwa maisha

Mahakama ya mjini Munich imemuhukumu kifungo cha maisha mtuhumiwa mkuu katika kesi iliyohusu vuguvugu la chini kwa chini la hapa nchini Ujerumani NSU Beate Zschaepe aliyekuwa mwanachama wa kundi hilo la Wanazi mamboleo.

Mahakama ilitoa uamuzi wake leo hii Jumatano ambapo Bibi Zschaepe amepewa hukumu hiyo ya kifungo cha maisha. Mshtakiwa huyo mkuu amekutwa na hatia kuhusiana na maujai ya watu 10 wengi wao wakiwa ni wahamiaji wa Kituruki ambao waliuwawa kwa kupigwa risasi kati ya mwaka 2000 na 2007.

Kesi hiyo ilisababisha mshtuko hapa nchini Ujerumani na ilisababisha pia malalamiko na lawama dhidi ya mashirika ya usalama ya nchini hapa ambayo yalilaumiwa kwa kuwa na ubaguzi katika kutoa huduma zake. Msemaji wa mahakama Florian Gliwitzky alisema haya baada ya mahakama kutoa uamuzi wake.

Beate Zschaepe mwenye umri wa miaka 43 hakuonyesha hisia zozote wakati Jaji aliyeongoza kesi hiyo Manfred Goetzl alipokuwa anasoma hukumu yake katika chumba cha mahakama kilichokuwa kimejaa huko mjini Munich. Mawakili wa bi Zschaepe wamesema watakata rufaa dhidi ya hukumu aliyopewa mteja wao.

Pamoja naye ni wanachama wengine wanne wa kundi hilo la kigaidi, Ralf Wohlleben ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kosa la kusambaza silaha zilizotumiwa kwenye mfululizo wa mauaji.

Mbele: Beate Zschaepe na wakili wake Mathias Grasel

Mbele: Beate Zschaepe na wakili wake Mathias Grasel

Mtuhumiwa wa tatu, ni Holger G, atakaetumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kuunga mkono kundi hilo la kigaidi. Wa nne ni Andre Eminger, ambaye amefungwa miaka miwili na miezi sita kwa kosa hilohilo la kuunga mkono kundi la kigaidi. Watu wanaounga mkono mrengo wa mkali wa kulia walipiga makofi kwa furaha kutokana na swahiba wao huyo kupewa adhabu ndogo ambayo hawakutarajia. Na mtuhumiwa ambaye ni wa tano ni Carsten S, ambaye alikuwa bado ni mvulana mdogo wakati wa uhalifu huo ulipofanyika, amepewa adhabu ya kuwekwa kizuizini kwa muda wa miaka mitatu kwenye jela ya watu wenye umri mdogo kwa kosa la kusaidia na kushabikia mauaji ya watu tisa.

Zschaepe alikamatwa mnamo mwaka 2011, muda mfupi baada ya washirika wake wawili kujiua. Pamoja na washirika wake hao Uwe Mundlos na Uwe Boehnhardt, waliunda kundi lililoendeleza itikadi ya watu weupe wenye chuki dhidi ya wahamiaji, hasa wa asili ya Kituruki.

Kundi hilo la NSU, liliikwepa polisi kwa karibu miaka 14 na yote haya ni kutokana makosa ya mara kwa mara yaliyofanywa na mashirika ya usalama hapa nchini Ujerumani na pia kutokana na wafuasi wa kundi hilo walilokuwa wanawapa taarifa za mapema.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPAE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga