Mjumbe wa Marekani azuru Afghanistan kufufua mchakato wa amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.05.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mjumbe wa Marekani azuru Afghanistan kufufua mchakato wa amani

Mjumbe maalum wa Marekani nchini Afghanistan amezitaka pande zinazohusika katika mgogoro nchini humo kupunguza machafuko, katika ziara ya kwanza tangu utawala unaozozana ulipofikia makubaliano ya kugawana madaraka.

Ziara ya mjumbe huyo inafanyika wakati kukiwa na ongezeko la ghasia ambazo zinatupiwa lawama kwa kiasi kikubwa kwa makundi yaliyo na mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS na ambayo yanalengwa kwenye mashambulizi ya mabomu ya Marekani.

Katika ujumbe wake kwenye ukurasa wa Twitter, Khalilzad aliwaeleza wawakilishi wa kundi la Taliban mjini Doha mwanzoni mwa wiki pamoja na rais Ashraf Ghani na kiongozi mwenza Abdullah Abdullah kwamba kulikuwa na haja ya kufufua makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwezi Februari baina ya Marekani na Taliban.

Khalilzad ametoa wito wa kupunguza machafuko kutoka pande zote kwenye mgogoro wa Afghanistan, ambao umevifanya vikosi vya Marekani kutumbukia kwenye mgogoro huo kwa miaka 19 sasa.

Pia ameongeza kuwa muda mwingi umepotea katika kuingia awamu ya pili na ya muhimu ya makubaliano hayo ambayo yanataka mazungumzo baina ya Taliban na utawala wa Afghanistan.

Abdullah atapaswa kuongoza juhudi hizo kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na Ghani ili kukomesha uhasama wa muda mrefu juu ya nani alishinda uchaguzi wa rais wa Afghanistan wa mwezi Septemba. Kiongozi huyo alikubali ushindi wa Ghani lakini kama sehemu ya makubaliano ya kugawana madaraka.

Katar Doha Unterzeichnung Abkommen USA Afghanistan Taliban Zalmay Khalilzad Abdul Ghani Baradar

Zalmay Khalilzad (kushoto) alipotia saini makubaliano ya amani pamoja na mwakilishi wa Taliban Mullah Abdul Ghani Baradar (kulia), Februari 29, 2020 mjini Doha, Qatar.

Rais wa Marekani, Donald Trump alitamka wiki iliyopita kwamba wanajeshi wa kimarekani walipelekwa kimakosa katika taifa hilo na kuitaka Afghanistan yenyewe kuzidisha juhudi.

Marekani inao askari wapatao 12,000 nchini Afghanistan, ambao wamegawanywa baina ya kikosi cha kupambana na ugaidi na wengine wakihudumu katika ujumbe wa Jumuia ya Kujihami ya NATO unaowapatia mafunzo na kulisaidia jeshi la nchi hiyo.

Marekani kwa hivi sasa inalipa kiasi cha dola bilioni 4 kwa mwaka kwa ajili kuendesha shughuli za wanajeshi wake nchini Afghanistan.

Hofu ya kuongezeka kwa vurugu za itikadi kali

Maafisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani wamelieleza shirika la habari la Associated Press kwamba wasiwasi wao mkubwa nchini Afghanistan ni kuongezeka kwa makundi yenye mafungamano na IS yenye makao yake makuu Mashariki.

Kundi hilo lina mafungamano na kundi la harakati za Kiislamu la Uzbekistan, kundi la Uighur la China, na lile la harakati za Kiislamu la Turkestan Mashariki.

Maafisa waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwa sababu ya unyeti wa suala hilo, wanadai kuwa makundi washirika ya IS nchini Afghanistan yanahusishwa na njama za mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Marekani.

Marekani pia inalituhumu kundi la IS kwa shambulizi baya kwenye hospitali ya akina mama mapema mwezi huu mjini Kabul ambalo liliwaua watu 24, wakiwemo watoto wawili wachanga na akina mama kadhaa.

Afghanistan Ashraf Ghani und Abdullah Abdullah

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani (kulia) na hasimu wake Abdullah Abdullah wamekubaliana tena kugawana madaraka baada ya mzozo wa miezi kadhaa.

Ongezeko la shughuli za IS nchini Afghanistan limeongeza uharaka kwa Marekani kuzidisha juhudi zake za kutekelezwa kwa mpango wa amani unaolitaka kundi la Taliban kupambana dhidi ya makundi ya kigaidi nchini humo.

Maafisa hao hao wa wizara ya ulinzi nao walisema kuwa wanalitaka kundi la Taliban kwenye mapambano dhidi ya IS kutoka ndani ya Afghanstan.

Kauli ya Taliban

Bila ya kuwepo mazungumzo ya ndani ya Afghanitsan, usitishaji mapigano ambao Marekani inautaka baina ya Taliban na serikali hauwezi kutokea.

Wawakilishi wa Taliban wanasema suala hilo la usitishaji mapigano litakuwamo kwenye ajenda ya mazungumzo ya ndani ya Afghanistan yaliyokuwa yamepangwa kuanza katikati mwa mwezi wa Machi.

Hata hivyo kucheleweshwa kwake kunaelekezwa kwa mzozano wa utawala wa Kabul na kuingiliwa kati kwa zoezi la kuwaachia wafungwa kama ilivyokubaliwa kwenye makubaliano.

Mjumbe huyo maalum wa Marekani ametaka zoezi la wafungwa kuachiwa kukamilika. Pia amesisistiza juu ya kuhitaji usaidizi wa Taliban katika kuwasaka Wamarekani waliopotea nchini Afghanstan akiwemo mhandisi Mark Frerichs aliyepotea mwezi Januari.

Chanzo: APE