1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjerumani wa IS ahukumiwa miaka 10 jela kwa kumuua binti

Grace Kabogo
25 Oktoba 2021

Mahakama moja mjini Munich imemuhukumu kifungo cha miaka 10 jela mwanamke wa Kijerumani baada ya kukutwa na hatia ya kuruhusu msichana wa jamii ya Yazidi mwenye umri wa miaka 5 kufa kutokana na kiu akiwa kwenye jua kali.

https://p.dw.com/p/42A2x
Deutschland | Prozess gegen Jennifer W.
Picha: Sebastian Widmann/Getty Images

Jaji kiongozi wa mahakama hiyo ya kusini mashariki mwa Ujerumani, Reinhold Baier amemuhukumu Jennifer Wenisch, mwenye umri wa miaka 30 ambaye alijiunga na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS katika moja ya kesi za kwanza kutolewa duniani inayohusiana na wapiganaji wa IS ambao waliwatesa watu wa jamii ya Yazidi. Wenisch amekutwa na hatia ya makosa mawili ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kumshikilia mtu kama mtumwa, kusaidia mauaji ya msichana kwa kutomuokoa pamoja na kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi. Msemaji wa mahakama hiyo, Florian Gliwitzky anafafanua zaidi kuhusu hukumu hiyo.

''Mahakama imemuhukumu kifungo cha miaka 9 kwa kifo cha mtoto kilichotokana na utumwa ambao unaangaliwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu na miaka miwili na miezi sita kwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi. Hii inafanya iwe jumla ya kifungo cha miaka 10,'' alisema Msemaji wa mahakama hiyo, Florian Gliwitzky anafafanua zaidi kuhusu hukumu hiyo.

Waliwanunua mama na binti yake

Mwanamke huyo pamoja na mumewe Taha A.-J., mwanachama wa IS walimnunua mwanamke wa Kiyazidi pamoja na mtoto wake. Waliwafanya watumwa, wakati wanandoa hao wanaishi Mosul mji uliokuwa unadhibitiwa na IS mwaka 2015.

Waendesha mashtaka wamesema baada ya mtoto kuugua na kukojolea godoro lake, mume wa mwanamke huyo alimfunga kwa minyororo nje kama adhabu na kuruhusu mtoto huyo kufa kwa kiu kutokana na joto kali. Mshtakiwa huyo alimruhusu mumewe kufanya hivyo na hakufanya lolote kumuokoa msichana huyo.

Irak Jesiden   Lalish Tempel Sinjar
Mwanamke wa Kiyazidi akiwa ameshika picha ya watu wa jamii ya Yazidi ambao wameteswa na ISPicha: AFP via Getty Images

Wenisch, kutoka mji wa Lohne ulioko kwenye jimbo la Lower Saxony aliyekuwa Mprotestanti, alibadili dini na kuwa Muislamu mwaka 2013. Mwaka 2014 alikwenda Iraq kupitia Uturuki na Syria kujiunga na IS. Waendesha mashtaka wamesema kazi ya mwanamke huyo aliyekuwa na bunduki ya AK-47, ilikuwa kuhakikisha wanawake wanafuata kanuni za kimavazi na tabia za kundi hilo lenye itikadi kali za Kiislamu. Mwanamke huyo alikamatwa na kurudishwa Ujerumani wakati akijaribu kupata nyaraka mpya za kitambulisho chake kwenye ubalozi wa Ujerumani mjini Ankara mwaka 2016.

Ashuhudia binti yake akifa

Akitambulika kwa jina lake la kwanza Nora, mama wa mtoto huyo alitoa ushahidi kwenye mahakama za Munich na Frankfurt kuhusu mateso yanayodaiwa kufanywa dhidi ya mtoto wake. Wakati akitoa ushahidi mama huyo amesema alilazimishwa kumuangalia binti yake akikata roho.

Soma zaidi: Ujerumani kuwasaidia Wayazidi

Mume wa Wenisch, pia anakabiliwa na mashtaka tofauti katika mahakama ya Frankfurt na hukumu yake inatarajiwa kutolewa mwezi Novemba. Taha alikamatwa nchini Ugiriki Mei mwaka 2019 baada ya Ujerumani kutangaza waranti wa kukamatwa kwake na alihamishiwa Ujerumani mwezi Oktoba. Kesi inayoendelea dhidi yake, ya kwanza dhidi ya mpiganaji wa zamani wa kundi la IS kuhusika na mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Yazidi imevutia hisia za kimataifa.

AFP, DW https://bit.ly/3EhWV67