Migomo na maandamano yatokota Ufaransa | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.10.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Migomo na maandamano yatokota Ufaransa

Vyama vya wafanyakazi vyaapa kuendeza mgomo.

default

Maafisa wa polisi wakipiga doria nchini Ufaransa. Waandamanaji 1400 wamekamatwa.

Serikali ya ufaransa imewatuma maafisa wa polisi kuondoa vizuizi vilivyowekwa barabarani na waandamanaji wanaopinga pendekezo la serikali la kuongeza mwaka wa kustaafu. Mgomo huo unavuruga uchumi wa taifa hilo la ulaya.

Vyama vya wafanyakazi vimeapa kuendelea na mgomo kuupinga muswada unaotarajiwa kupigiwa kura na baraza la Senate la Ufaransa wiki hii. Mabadiliko hayo ya mfumo wa kustaafu yamezua mtafaruku nchini humo. Theluthi moja ya vituo vya mafuta vimefungwa aidha kwa kukosa au kupungukiwa na mafuta. Ufaransa ina takriban vituo 12,500 vya mafuta. Waziri wa ndani, Brice Hortefeux amesema maeneo ya kuhifadhia mafuta yaliyokuwa yamefungwa yalifunguliwa jana usiku huku mgomo huo ukiendelea kutokota.

Vyama vya wafanyakazi vinavyoungwa mkono na Wafaransa wengi vinajaribu kumshinikiza rais Sarkozy ambaye umaarufu wake uko katika kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha miezi 18, atupilie mbali muswada huo unaotizamwa kama mtihani mkubwa kwa uongozi wake.

Serikali yake inayoegemea katika siasa za wastani za mrengo wa kulia, imesimama kidete dhidi ya msururu wa migomo na maandamano tangu msimu wa joto na yaliyoshika kasi wiki iliyopita.

Msemaji wa serikali ya Ufaransa, Luc Chatel alisema katika mahojiano ya kituo cha redio cha RTL kwamba kuandamana ni kitu kimoja na kufunga barabara ni kitu kingine. Akiikariri amri ya rais Sarkozy kwa idara ya polisi, msemaji huyo alisema hawatakubali taifa lizuiwe.

Finanzkrise in Frankreich: Präsident Sarkozy will Arbeitsplätze retten

Rais Nikolas Sarkozy wa Ufaransa. Wachunguzi wanasema hali iliopo nchini mwake ni mtihani mkubwa kwa serikali.

Kiasi ya watu milioni moja waliandamana jana nchini humo, ikiwa ni maandamano ya sita ya kitaifa tangu mwezi Juni katika kile kinachotizamwa kama changamoto kubwa katika mabadiliko ya kiuchumi yanayotekelezwa katika bara la ulaya linalozongwa na mzozo wa kiuchumi.

Visa vichache vya ghasia vilizuka katika maandamano yaliyofanyika katika mji wa Lyon huku viongozi wakiingiwa na wasiwasi kwamba vikundi vya watu vinajaribu kuvuruga maandamano yanayonuiwa kuwa ya amani. Waandamanaji pia walifunga barabara ya kuelekea katika viwanja vya ndege vya Toulouse na Bordeaux huku malori yakitumiwa kuzuia barabara na kusababisha msongamano wa magari.

Kulingana na utafiti uliochapishwa leo na gazeti la Les Echos nchini humo, Wafaransa wengi wanayaunga mkono maandamano hayo. Asilimia 59 ya wale waliohojiwa walisema wanavitaka vyama vya wafanyakazi viendelee kuishinikiza serikali kutopitisha muswada huo unaotarajia kuongeza mwaka wa kustaafu kutoka 60 hadi 62 ifikapo mwaka wa 2018. Muswada huo tayari umepitishwa na bunge la Ufaransa na unatarajiwa kupigiwa kura katika baraza la Seneti kabla ya Jumapili.

Waziri wa ndani, Hortefeux alisema katika kipindi cha wiki moja kiasi ya watu 1, 423 wengi wao wakiwa watoto, wamekamatwa baada ya maandamano kukumbwa na ghasia katika miji kadhaa.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters/ AP/DPA

Mhariri, Aboubakary Liongo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com