Miaka 10 ya Ban Ki-moon usukani mwa UN | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Miaka 10 ya Ban Ki-moon usukani mwa UN

Ban Ki-moon anamaliza uongozi wake ndani ya Umoja wa Mataifa akilia na migogoro inaoendelea duniani lakini akijivunia makubaliano ya kimataifa ya mabadiliko ya tabia nchi na malengo mapya ya maendeleo ya UN.

Akitazama nyuma katika kipindi cha uongozi wake wa shirika la Umoja wa Mataifa (UN) katika mkutano wa waandishi habari mapema mwezi Desemba, Ban aliwaambia wandishi habari kuwa "huu umekuwa muongo wa mtihani usiokwisha".

Wakati ameshuhudia hatua za pamoja zikiboresha maisha ya mamilioni ya watu, Ban alieleza kuvunjwa moyo na kushindwa kumalizwa vita vya Syria, ambavyo viko katika mwaka wake wa sita sasa, na migogoro nchini Sudan Kusini, Yemen, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kwingineko.

Na katika ukosoaji usio wa kawaida wa viongozi wa dunia, aliwalaumu marais ambao hakuwataja, mawaziri wakuu na wafalme kwa machafuko yanayoikumba dunia hivi sasa - na kueleza kukatishwa tamaa kwamba wengi wanajali zaidi kubakia madarakani kuliko kuboresha maisha ya wananchi wao. Aliitaja hasa Syria, akisema haelewi kwa nini inaendelea kushikiliwa mateka kwa hatma y amtu mmoja, Bashar Assad.

Hata baada ya kuondoka Umoja wa Mataifa, Ban alisema ataendelea kuwasihi viongozi wapya na wa muda mrefu kukubaliana na ukweli wa karne ya 21, kwamba "ushirikiano wa kimataifa ndiyo unabakia kuwa njia kuelekea ulimwengu wa amani na wenye mafanikio", na kuonesha "uongozi wa huruma."

UN Generalversammlung - Antonio Guterres, Vereidigung als Generalsekretär in New York (Reuters/L. Jackson)

Ban Ki-moon akiwa na mrithi wake, katibu mkuu mpya Antonio Guterres katika makao makuu ya UN mjini New York Desemba 12, 2016 baada ya Guterres kuapishwa.

Ili kutilia mkazo hilo, ziara ya mwisho ya katibu mkuu Ban mwezi Desemba ilikuwa katika Maktaba ya rais Abraham Licoln na kumbukumbu yake mjini Springfield, Ilinois. "Lincoln alikuwa shujaa wa usawa, ushirikishwaji na maridhiano, na tunahitaji moyo huo vibaya mno leo," Ban alisema kuhusu kiongozi huyo aliekuwa rais wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani.

Mamlaka halisi ya Katibu mkuu

Ban pia alielezea kuvunjwa moyo na namna Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi na matarajio katika baadhi ya maeneo ya dunia kwamba katibu mkuu ana nguvu, za kuwa hata "mtu mwenye mamlaka ya juu kabisaa." Hilo haliwezekani, aliliambia shirika la habari la Associated Press (AP) mwezi Septemba, kwa sababu mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa yanafanya maamuzi na katibu mkuu huyatekeleza. Katibu mkuu wa UN hawezi kutekeleza sera au mikakati yake mwenyewe.

John Bolton, aliekuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa wakati Ban alipoteuliwa kuwa katibu mkuu, alisema utawala wa rais George W. Bush ulimuunga mkono kwa sababu "tulitaka mtu ambaye angefanya kile nchi wanachama zinachotaka" - na siyo kujichukulia maamuzi juu ya masuala na pia kufanya kazi kama mwanadiplomasia wa juu wa dunia kama alivyokuwa wakati huo katibu mkuu Kofi Annan.

"Nadhani Ban Ki-moon ametimiza matarajio yetu, ambayo siyo kusema kwamba nilikubaliana na kila msimamo aliouchukuwa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na vitu kama hivyo," Bolton aliliambia shirika la AP.

Wakati waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Korea Kusini, aliekuwa wakati wa vita Korea, alipochukuwa wadhifa wa katibu mkuu kutoka kwa Kofi Annan mwanzoni mwa 2007, aliahidi uongozi wake ungefanya juhudi na kujenga madaraja na kuondoa migawiko." Na hapo ndipo akalifanya suala la kukabiliana na nogezeko la joto la dunia, lisilokuwa muhimu, kuwa kipaumbele chake cha juu.

UN Generalversammlung - Antonio Guterres, Vereidigung als Generalsekretär in New York (picture-alliance/dpa/J. Lane)

Katibu mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akila kiapo chan wadhifa huo mjini New York Desemba 12, 2016.

Wakati wa muhula wake wa kwanza alipongezwa kwa kusaidia kulipeleka suala la mabadilko ya tabia nchi karibu na juu kwenye ajenda ya kimataifa, kwa kuunda kitengo cha wanawake wa Umoja wa Mataifa (UN Women) kupambana na ukosefu wa usawa wa kijinsia, na kwa kupaza sauti mapema na kwa nguvu kwa ajili ya waandamanaji nchini Tunisia na mataifa mengine yaliosimama dhidi ya tawala katika uasi wa umma - maarufu kama Machipuko ya Arabuni.

Wakati wa muhula wake wa pili, kampeni yake ya makubaliano mapya ya tabia nchi ilizaa mkataba wa Paris mwezi Desemba 2015. Alizishawishi nchi zote 193 wanachama kukubaliana juu ya Malengo mapya 17 ya Umoja wa Mataifa na shabaha 169 za kukabiliana na umaskini, kufikia usawa wa kijinsia, kulinda mazingira na kuhakikisha utawala bora kufikia mwaka 2030. Alitoa wito wa mapema kukomeshwa kwa vita vya Syria, na uliunga mkono kwa nguvu haki za mashoga licha ya upinzani mkali kutoka mataifa mengi.

Ukosoaji dhidi yake

Lakini Ban pia alikabiliwa na ukosoaji - katika muhula wake wa kwanza kwa kutozungumzia juu ya ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini Urusi na China. Katika muhula wake wa pili, namna Umoja wa Mataifa ulivyoshughulikia mripuko wa Ebola nchini Haiti, na kushindwa kwake kushughulikia ipasavyo udhalilishaji wa kingono uliodaiwa kufanywa na walinda amani wake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kwingineko vilikosolewa sana duniani.

Hatua ya Ban kuuondoa kwa muda, muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen kutoka orodha "nyeusi" kwa madai ya kuuwa watoto baada ya muungano huo kutishia kuacha kufadhili programu nyingi za UN ilikosolewa pia. Ban amabye ni mtu wa kazi, alisafiri zaidi ya watangulizi wake wote kwenye kazi za UN.

Alisema viongozi wengi wa nchi za Magharibi wanzungumza kupitia taarifa, lakini yeye anaamini mikutano ya ana kwa ana na viongozi wa dunia ni muhimu kupata uungwaji mkono kukomesha migogoro au kuchochea hatua kuhusu masuala kama mabadiliko ya tabianchi na kupambana na umaskini.

Myanmar Kofi Annan (Reuters/W. Lone)

Mtangulizi wa Ban, Mghana Koffi Annan, ambaye kwa sasa ni mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anaeshughulikia mgogoro wa Jamii ya Warohingya nchini Myanmar.

Licha ya uongozi wake wa muongo mzima ndani ya Umoja wa Mataifa, Ban siyo mtu anaefahamika sana. Amekosolewa kwa kushindwa utashi na mbinu za mawasiliano zinazohitajika katika ulimwengu unaozidi kuwa wa utandawazi, inagwa faraghani na kwenye tamasha la kila mwaka la chama cha waandishi wa habari za Umoja wa Mataifa, amekuwa akionesha ustadi wa ucheshi.

Suala la Korea Kaskazini

Wakati Ban alipoingia katika Umoja wa Mataifa, alikuwa mstiari wa mbele katika majadiliano ya nyuklia kati ya Korea Kusini na Kaskazini. Alisema alipanga kusafiri kwenda Pyongyang kama katibu mkuu, kitu ambacho Anna hakuwahi kufanya, lakini hakufika huko.

Matumaini yake ya kutumia nafasi yake ya UN kuendeleza amani na maridhiano katika rasi ya Korea, na utatuzi wa amani wa suala la Nyulika ya Korea, limeendelea kuwa njozi. Lakini baada ya kupumzika kwa muda, atarudi nchini Korea Kusini wakati amabpo kuna uvumi mkubwa kwamba atakuwa mgombea wa urais kuchukuwa nafasi ya rais wa nchi hiyo anayekabiliwa na mchakato wa kuvuliwa madaraka. Ikiwa itakuwa hivyo, Korea Kaskazini itakuwa ya juu kwenye ajenda yake.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Yusra Buwayhid

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com