1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme Charles III alihutubia bunge la Ujerumani

Daniel Gakuba
30 Machi 2023

Mfalme Charles III wa Uingereza yuko nchini Ujerumani katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aliporithi kiti cha enzi. Leo Alhamisi amelihutuia bunge mjini Berlin, na kusifu msaada wa Ujerumani kwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4PVSh
König Charles Rede Bundestag
Mfalme Charles III wa Uingereza akilihutubia Bunge la Ujerumani (Bundestag)Picha: Wolfgang Kumm/dpa/picture alliance

Kabla ya hotuba yake bungeni, Mfalme Charles III alipokelewa kwa mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ikiwa siku ya pili ya ziara yake inayohitimishwa kesho.

Soma zaidi: Mfalme wa Uingereza Charles lll aanza ziara ya kiserikali nchini Ujerumani

Hotuba yake katika bunge la Ujerumani, Bundestag ameitoa kwa lugha za Kiingereza na Kijerumani, akiwashukuru Wajerumani kwa upendo walioionyesha familia yake kufuatia kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth II Septemba mwaka jana. Amesema ziara yake inalenga kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi mbili.

Kisha, Mfalme Charles III ameisifu Ujerumani kwa ukarimu wake wa kuisaidia Ukraine kuweza kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Asifu msaada mkubwa wa Ujerumani kwa Ukraine

Amesema uamuzi wa Ujerumani kuipatia Ukraine msaada mkubwa wa kijeshi ni wa ushujaa usio na kifani, na kuongeza kuwa kwa pamoja Ujerumani na Uingereza zimetoa mchango muhimu wa uongozi, wakati huu Ulaya inapokabiliwa na kitisho.

Deutschland König Charles zu Besuch in Berlin
Kutoka kulia kwenda kushoto: Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Mfalme Charles III wa Uingereza, Camilla; mke wa Mfalme Charles III, na Elke Buedenbender; mke wa Rais Steinmeier.Picha: Phil Noble/REUTERS

''Usalama wa Ulaya, na pia maadili yetu ya kidemokrasia vinakabiliwa na kitisho. Lakini dunia haikukaa tu na kutazama. Tumetikiswa na uhalifu mbaya lakini tunaweza kufarijiwa na umoja wetu katika kulinda uhuru na usalama wa Ukraine,'' amesema Mfalme Charles III.

Soma zaidi: Mfalme Charles III kulihutubia bunge la Ujerumani katika ziara yake ya kwanza

Ziara ya mfalme huyo anayeambatana na mke wake Camilla imesheheni shughuli nyingi. Asubuhi ya leo, kando na kupokelewa na Kansela Olaf Scholz, amesaini kitabu cha wageni maarufu wanaouzuru mji wa Berlin, na kulitembelea soko la siku moja kwa wiki katika mji huo mkuu.

Ratiba yake kuanzia alasiri inajumuisha ziara katika kambi ya wakimbizi kutoka Ukraine kwenye uwanja wa zamani wa ndege, akisindikizwa na rais wa shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, na mazungumzo na wahandisi wa kijeshi wanaounda bataliani moja wakitoka Ujerumani na Uingereza iliyoko katika kambi ya Finowfurt kaskazini mashariki mwa Berlin.

Deutschland | King Charles III besucht Berlin
Mfalme Charles III alipokelewa mjini Berlin kwa heshima zote za kijeshi. Kulia kwake ni Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: WOLFGANG RATTAY/AFP

Suala la kutunza mazingira ni muhimu kwa Mfalme Charles III

Atakitembelea pia kijiji rafiki kwa mazingira, ambako atashiriki katika utengenezaji wa jibini na kufanya mjadala juu ya kilimo kisichotumia mbolea ya viwandani, mojawapo ya masuala muhimu sana kwa mfalme huyo wa Uingereza.

Soma zaidi: Mfalme Charles kuzuru Ujerumani na Ufaransa

Ingawa Ujerumani imekuwa nchi ya kwanza kuitembelea baada ya kurithi kiti cha ufalme, Charles III alikuwa ameichagua kwanza Ufaransa, lakini ziara yake huko ikaahirishwa kutokana na maandamano yenye vurugu kupinga mageuzi yanayofanywa na rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron katika mfumo wa pensheni.

Japo Wajerumani wengi wamemkaribisha kwa furaha mfalme huyo, baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa kushoto wamesema ni aibu kwa taasisi ya kidemokrasia kama bunge la Ujerumani, kumpa jukwaa mfalme, ambaye wanasiasa hao wanamchukulia kama mwakilishi wa utawala kandamizi uliopitwa na wakati.

 

Vyanzo:/rc/sms (dpa, AFP, Reuters, AP)