Merkel kuzungumza tena na wanamazingira | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel kuzungumza tena na wanamazingira

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ataongoza duru ya pili ya mazungumzo na chama cha watetezi wa mazingira Die Grüne Jumanne hii, juu ya uwezekano wa kuundwa kwa kile ambacho kinaweza kuwa mseto wa kihistoria.

Kansela Angela Merkel na wajumbe wa muungano wake wakiwasili kwa ajili ya mazungumzo na chama cha die Grüne mjini Berlin.

Kansela Angela Merkel na wajumbe wa muungano wake wakiwasili kwa ajili ya mazungumzo na chama cha die Grüne mjini Berlin.

Mkutano huo unafanyika siku moja baada ya Merkel na viongozi wa muungano wa Merkel wa kihafidhina unaoongozwa na chama chake cha Christian Democratic Union CDU, kukubaliana kufanya duru ya tatu ya mazungumzo na chama kikuu cha upinzani cha Social Democrats SPD siku ya Alhamisi.

Hata hivyo, katibu mkuu wa chama cha CDU Hermann Groehe alisisitiza kuwa mazungumzo na wanamazingira yatachukuliwa kwa uzito mkubwa. CDU na ndugu zao wanaoongoza jimbo la Bavaria, Christian Social Union CSU, walipata ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi uliopita.

Wajumbe wa SPD wakiwa mjini Berlin kwa ajili ya mazungumzo na muungano wa Merkel.

Wajumbe wa SPD wakiwa mjini Berlin kwa ajili ya mazungumzo na muungano wa Merkel.

Ni mazungumzo ya utafiti tu
Lakini Merkel anahitaji mshirika mpya wa kuunda naye serikali baada ya chama cha Waliberali FDP, walichoshirikiana nacho katika miaka minne iliyopita, kushindwa kuingia bungeni, na muungano wake wa CDU na CSU kushindwa kupata wingi wa kutosha kuuwezesha kuunda serikali kivyake.

Muungano wa Merkel ulifanya mazungumzo yaliyodumu kwa masaa nane na SPD mjini Berlin, na katibu mkuu wa CDU Herman Groehe alisema uamuzi rasmi kuhusu duru ya tatu ya mazungumzo utatangazwa baadae hii leo, baada ya mazungumzo na die Grüne.

Katibu mkuu wa chama cha SPD Andrea Nahles alisema mazungumzo na CDU yalishadidi sana. "Kwa baadhi ya mada tunaona tunaelekea sehemu moja, kwa nyingine tunatofautiana, kwa mfano kuhusu kima cha chini cha mshahara au kodi, alisema Nahles baada ya kukamilika kwa duru ya pili.

Lakini katibu mkuu wa CDU Hermann Groehe alisema mazungumzo ya sasa hayalengi kupata tahfifu madhubuti. "Mazungumzo ya utafiti si sehemu ya kutafuta tahfifu thabiti, lakini kuona iwapo inaleta maana kushiriki na upande mwingine katika majadiliano ya kuunda muungano. Kwa hivyo kwangu mazungumzo ya sasa siyo ya kusikiliza yale yanayotuunganisha au tunayotofautiana."

Wajumbe wa chama cha Kijani wakiwasili kwa ajili ya mazungumzo na muungano wa Merkel.

Wajumbe wa chama cha Kijani wakiwasili kwa ajili ya mazungumzo na muungano wa Merkel.

Raia wapendelea muungano mkuu
Merkel anatumai kuamua wiki hii ni chama gani anataka kuazisha nacho mazungumzo rasmi ya kuunda serikali. Ushirikiano na chama cha die Grüne, kilichopata asilimia 8.4 ya kura mwezi Septemba itakuwa mara ya kwanza kwa wahafidhina na wanamazingira kugawana madaraka kwa ngazi ya taifa nchini Ujerumani. Lakini tofuati kubwa bado zipo kati ya CDU/CSU na chama cha Kijani, zikiwemo juu ya kuendeleza matumizi ya nishati rafiki na mazingira, na katika maeneo kama vile sera ya wakimbizi na haki za mashoga.

Baada ya mkutano wao wa kwanza na Merkel wiki ilyiopita, viongozi wengi wa Kijani wana mashaka iwapo mazungumzo ya leo yatasababisha awamu nyingine na CDU na CSU. Mwenyekiti wa chama cha CSU na waziri mkuu wa jimbo la Bavari Horst Seehofer, wiki hii alirejelea tena kuelezea kupendelea kwake kuunda serikali ya muungano mkubwa na SPD, kuliko kuungana na wanamazigira.

Uchunguzi wa maoni uliofayika hivi karibuni umeonyesha kuwa theluthi mbili ya Wajerumani wangependelea muungano kati ya vyama vikuu viwili - yaani muungano wa Merkel na SPD.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman