Merkel achaguliwa tena kuongoza CDU | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel achaguliwa tena kuongoza CDU

Kansela Angela Merkel amechaguliwa tena kuendelea kukiongoza chama cha CDU, huku dalili zikionesha kuwa kiongozi huyo mashuhuri anaweza asiwe na mpinzani hata kama akiamua kugombea tena ukansela.

Kansela Angela Merkel akipongezwa baada ya kutangazwa kuongoza tena chama chake cha CDU.

Kansela Angela Merkel akipongezwa baada ya kutangazwa kuongoza tena chama chake cha CDU.

Akiwa amefurahishwa kupita kiasi na matokeo yaliyompa ushindi asilimia 96.7 kuongoza tena chama chake, Angela Merkel anaonekana kama nyota isiyofifia nuru yake kwenye CDU.

"Tunapaswa kukimbia na hatupaswi kukaa siku nzima kuwaza matatizo yetu. Ili tuseme tunataka viwango, tunapaswa kuwa wa mwanzo kuviweka viwango hivyo na sio wa mwisho. Dunia haitungojei sisi", alisema kwenye hotuba yake ya kushukuru kuchaguliwa tena, ilijaa falsafa za kiuchumi na ujasiri wa kiuongozi, katika namna ambayo wengi walisema hawajawahi kumuona Angie, jina la utani la Kansela Merkel miongoni mwa wafuasi wake, akiwa kwenye hamasa hiyo.

Kwa kila hali, mkutano huu mkuu wa chama umeimarisha zaidi nguvu za Merkel, ambazo tangu hapo awali hazina mpinzani. Hotuba yake hiyo ilivuuka mipaka ya siasa za ndani, na kuingia hadi kwenye anga za kimataifa, kama vile suala la mzozo wa Urusi na Ukraine, uhusiano wa Ujerumani na Marekani, na pia mustakabali wa Umoja wa Ulaya, ambao Ujerumani inachukuliwa kama kinara wake mkuu.

Mzozo wa Ukraine

Juu ya mzozo wa Ukraine, kauli yake ilibakia pale pale pa siku zote, kwamba Urusi ikome kukiuka sheria za kimataifa na kwamba vikwazo dhidi ya Moscow viongezwe.

Wanachama wa CDU wakipiga kura kumchagua kiongozi wao.

Wanachama wa CDU wakipiga kura kumchagua kiongozi wao.

"Lengo letu ni kuwa na mamlaka ya Ukraine isiyoingiliwa, iliyo huru na ambayo inaweza kujiamulia yenyewe mustakabali wake," alisema Merkel.

Kiongozi huyo wa CDU alitumia hotuba hiyo ya dakika 80 kuwapa kile ambacho wajumbe wa mkutano huo mkuu walitaka kukisikia, yakiwemo mashambulizi makali dhidi ya chama mwenza kwenye serikali ya muungano, SPD, hasa baada ya chama hicho kwenye jimbo la Thüringen kuonesha dalili za kuungana na chama cha upinzani cha Die Linke kuunda serikali.

Akizungumzia kupanda kwa haiba ya Merkel kwenye mkutano huo wa 27 wa CDU, Rais wa Chama cha Watu wa Ulaya, Joseph Daul, aliwaambia wajumbe wanapaswa kujifaharisha kwa kuwa na kiongozi wa aina ya Merkel.

Miongoni mwa sifa anazomwagiwa kimataifa ni kujipambanua kwake na viongozi wa mataifa mengine makubwa, kwa kutopendelea kusafiri akiwa na misafara ya ulinzi mkali wa kijeshi kama ilivyo kwa Rais Barack Obama wa Marekani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Kay-Alexander Scholz
Mhariri: Saumu Yusuf

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com