1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May anusurika kura ya kutokuwa na imani naye

Caro Robi
13 Desemba 2018

 Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amenusurika kura ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa wabunge wa chama chake cha Conservative.

https://p.dw.com/p/39zsh
UK Ministerpräsidentin Theresa May
Picha: picture-alliance/newscom/H. Philpott

Wabunge 200 dhidi ya 117 wamepiga kura kumuunga mkono kusalia kuwa kiongozi wa chama hicho  na waziri mkuu, lakini hiyo inamaanisha amepoteza uungwaji mkono wa theluthi moja ya wabunge wa chama chake na hivyo kuashiria bado anakabiliwa na changamoto kubwa kutekeleza mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiengua kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya ujulikanao Brexit.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, May amesema amefurahi kupata uungwaji mkono wa wanachama wenzake wa Conservative katika kura hiyo iliyopigwa jana usiku.

Bado May anakabiliwa na changamoto

Lakini mbunge Jacob Rees Mogg mmoja wa wabunge 48 waliowasilisha barua ya kutaka kura hiyo ya kutokuwa na imani na uongozi wa May amesema matokeo hayo ni ya kusikitisha akisitiza May anahitaji kujiuzulu mara moja.

England House of Commons EU Brexit Theresa May
Wabunge wa Uingereza wakimsikiliza Waziri mkuu Theresa MayPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Duffy

Kabla ya kura hiyo, May aliwaahidi wabunge wa chama chake kuwa hatawania muhula mwingine wa kukiongoza chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022.

Sasa kiongozi huyo hawezi kukabiliwa na kura nyingine ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa chama chake kwa kipindi cha mwaka mmoja, lakini iwapo atashindwa katika kura ya wabunge wote 650 wa Uingereza mwezi ujao, serikali yake bado inaweza kukabiliwa na kura ya kutokuwa na imani nayo.

Rees Mogg na wabunge wengine wenye misimamo mikali hawajafurahishwa kabisa na makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya May na Umoja wa Ulaya mwezi uliopita, wakihofia kuwa Uingereza itajikuta ikiwa na mahusiano ya karibu na umoja huo kwa miaka mingi baada ya nchi hiyo kujiengua rasmi kuwa mwanachama tarehe 29 Machi mwakani.

Wanaomuunga mkono wanasema matokeo hayo yanaonesha kuwa sasa chama kinahitaji kumuunga mkono kikamilifu, lakini wanaompinga wanaona makubaliano aliyoyafikia na Umoja wa Ulaya kuwa usaliti wa malengo ya kura ya maoni ya 2016 na kumtaka ajiuzulu.

Viongozi wa EU wasisitiza hakutakuwa na majadiliano mapya

Mnamo Jumatatu wiki hii, May aliahirisha kura bungeni kuhusu rasimu ya makubaliano aliyoyafikia akihofia kushindwa vibaya. Ameahidi kura hiyo itafanyika kabla ya tarehe 21 Januari ambapo huenda akashindwa na kuutumbukiza mchakato wa Brexit katika mzozo mwingine.

EU-Sondergipfel zum Brexit in Brüssel
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na MayPicha: Reuters/O. Hoslet

Leo Alhamisi, waziri huyo mkuu wa Uingereza anaelekea Brussels kuhudhuria mkutano maalum wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, ambako atajaribu kuwashawishi viongozi wenzake kulegeza kamba kuhusu makubaliano ya Brexit ili aweze kutumia kuwashawishi wabunge walio na mashaka kuhusu mpango wake.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameonesha uelewa kwa changamoto anazokumbana nazo May lakini wamesisitiza hakutakuwa na mazungumzo mengine ya kubadilisha yaliyofikiwa mwezi uliopita baada ya takriban miaka miwili ya mazungumzo magumu.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel hapo jana amesema bado anatumai kuwa Uingereza itaondoka kutoka Umoja wa Ulaya kwa njia ya mpangilio lakini hakuna nia ya kubadilisha makubaliano ya Brexit yaliyofikiwa. Suala tete linalozua mashaka ni kuhusu Ireland Kaskazini.

Viongozi wa Ulaya wanajitayarisha kwa lolote lile ikiwemo Uingereza kuondoka bila ya kufikiwa makubaliano au hata kufanyika kwa kura nyingine ya maoni Uingereza kuhusu Brexit.

May mwenye umri wa miaka 62, aliyeingia madarakani baada ya kura hiyo ya maoni ya 2016 ameahidi kutekeleza kikamilifu Brexit, kudumisha mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya na kuliunganisha taifa lililogawanyika.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp