Mauaji ya Minneapolis yazusha maandamano
26 Januari 2026
Serikali ya Marekani inazidi kukabiliwa na shinikizo kuhusiana na hatua yake ya kuwaandama wahamiaji, na hasa baada ya matukio ya kuuwawa kwa watu kadhaa na maafisa wa shirika la ulinzi wa mipaka la nchini humo ICE.
Hali imechafuka zaidi katika jimbo la Minnesota hasa katika mji wa Mineapolis baada ya kuuwawa siku ya Jumamosi mtu mmoja aliyetajwa kwa jina Alex Pretty mwenye umri wa miaka 37 anayefanya kazi ya uuguzi kwenye wodi ya wagonjwa mahututi.
Kutokana na matukio yanayosababishwa na maafisa wa ICE utawala wa jimbo hilo la Minessota na uongozi wa miji ya Minneapolis na St Paul ulifunguwa kesi dhidi ya wizara ya mambo ya ndani ya Marekani mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kisa cha kupigwa risasi na kuuliwa Renee Good.
Hivi leo jaji wa mahakama ya shirikisho anasikiliza hoja zinazotolewa ikiwa harakati hizo za kuwaandama wageni katika jimbo la Minnesota zinapaswa kusitishwa kwa muda au la.
Mwanasheria mkuu wa jimbo la Minessota,ambaye ni Mdemocrat Keith Ellison amesema atahudhuria kesi hiyo hivi leo na wanamtaka jaji Kathleen Menendez kuamuru mashirika ya usalama ya serikali kupunguza idadi ya maafisa na mawakala wanaoendesha harakati za kuwaandama wageni katika jimbo hilo na kuendesha mipango hiyo kwa kiwango kilichokubaliwa kisheria. Chuki dhidi ya Wageni
Maandamano yamefanyika Jana kufuatia kuuwawa Jumamosi kwa raia wa Marekani Alex Pretty kwa kupigwa risasi wakati akipambana kujiokowa kutoka mikononi mwa maafisa wa ulinzi wa mipaka.
Wakaazi wa Minneapolis walikusanyika Jumapili kwenye eneo yalikofanyika mauaji hayo huku baadhi wakisimulia namna walivyojawa na hasira na uchungu kutokana na tukio hilo.
"Niko hapa kwasababu siamini kwamba hakuna mtu asiyetakiwa kuwa hapa na nafikiri namna serikali inavyoleta maafisa wa ICE kuwachukuwa majirani zetu na kuzitenganisha familia sio ubinadamu kabisa.Na ikiwa hatutozungumza basi hakuna atakayesema kitu. Kwahivyo ndio sababu tuko hapa kusimama kwaajili ya jamii yetu''
Viongozi mbali mbali nchini Marekani wameonesha kughadhabishwa na namna matukio hayo yanavyoendelea kusababisha wasiwasi nchini humo. Marais wa zamani Barack Obama na Bill Clinton jana Jumapili waliwataka wamarekani kusimama kidete kutetea maadili ya taifa lao.
Maandamano ya kupinga mauaji ya Renee Good nchini Marekani
Utawala wa rais Donald Trump ambao umekuwa ukiilaumu serikali iliyoondoka ikiongozwa na Wademocrats kwamba ndio chanzo cha kushuhudiwa mparaganyiko wa kijamii nchini humo,umedai kwamba Pretti aliyeuwawa Jumamosi alidhamiria kuwadhuru maafisa wa ICE kwasababu aliwanyooshea bastola, wanayodai walimpokonya kabla ya kumuua.
Hata hivyo video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na vyombo vya habari inamuonesha Pretti hakuwa hata mara moja kuikamata bastola.
Huku hali ya wasiwasi ikiongezeka Minneapolis, rais Barack Obama na mkewe Michelle wamesema kupitia taarifa iliyotolewa jana kwamba kuuwawa kwa kupigwa risasi Pretti ni tukio linalopaswa kuwaamsha Wamarekani kutambuwa kwamba misingi iliyoijenga nchi yao inazidi kuvurugwa.